Wednesday, April 4

Diamond, Samatta watakiwa nchini Marekani kutunukiwa tuzo


Moshi. Watanzania watatu na raia wa Marekani, wameteuliwa kutunukiwa tuzo katika tamasha lililoandaliwa na Watanzania waishio ughaibuni (Diaspora) litakalofanyika Dallas nchini Marekani.
Miongoni mwa watakaopewa tuzo ni Dk Steve Meyer ambaye ni daktari bingwa katika Hospitali ya Mercy iliyopo jiji la Sioux, Marekani aliyewatibu manusura wa ajali ya wanafunzi wa Lucky Vincent.
Katika ajali hiyo iliyotokea Mei 2017 eneo la mlima Rhotia wilayani Karatu mkoani Arusha, wanafunzi 32, walimu wawili na dereva walipoteza maisha katika ajali hiyo.
Mei 14, 2017, shirika la Samaritan Purse liliwapeleka manusura wa ajali hiyo, Doreen Mshana, Saidia Awadhi na Wilson Tarimo nchini Marekani na kurejea nchini Agosti 17 baada ya matibabu.
Akizungumza na gazeti hili kutoka Dallas jana, mratibu wa tamasha hilo, Ben Kazora alisema wanampa tuzo daktari huyo kwa kutambua mchango wake katika kuokoa maisha ya watoto hao.
“Sote tunatambua namna ajali ilivyokuwa mbaya na ilivyopoteza wapendwa wetu wengi. Dk Meyer na timu yake walifanya kila njia kuokoa maisha ya watoto wale watatu walionusurika,” alisema.
Kazora anayeishi Dallas, Texas aliwataja wengine walioteuliwa kupewa tuzo hiyo ni mwanamuziki wa kizazi kipya, Nassib Abdul maarufu Diamond Plutnumz na mwanasoka wa kimataifa, Mbwana Samatta.
“Tunampa Diamond zaidi kwa kutumia kipaji chake cha muziki kuitangaza nchi kitaifa na kimataifa, vivyo hivyo Samatta kwa kutumia kipaji chake cha kusakata kabumbu kuitangaza Tanzania,” alisema.
Kwa mujibu wa Kazora, mwingine ni mwanariadha John Akhwari ambaye mwaka 1968, alimaliza mbio katika michezo ya Olympic iliyofanyika Mexico City licha ya kuumia mguu.
Naye meya wa Dallas Texas nchini Marekani, Mike Rawlings aliwakaribisha Watanzania hao kushiriki tamasha la Tanzania Day, litakalofanyika jijini humo kwa lengo la kutangaza fursa za biashara na utalii.
Akizungumza kwa simu na gazeti hili, Rawlings alisema kwamba tamasha hilo linafahamika kwa jina la “Tanzania Day”, litafanyika Dallas na kuwakutanisha Watanzania na Wamarekani kwa ajili ya kubadilishana fursa za uchumi.

No comments:

Post a Comment