Mzee alisema hivi sasa Zanzibar nzima kuna mawakili 57 tu ambao wanashughulikia kesi zote za Unguja na Pemba, kiwango ambacho ni kidogo ikilinganisha na idadi ya kesi zinazofunguliwa.
Hata hivyo, Mzee hakutaja kiwango cha mawakili wanaowahitaji ili kufikia malengo yao.
Alisema malalamiko ya baadhi ya kesi hizo kuchelewa kutolewa uamuzi, linaweza kumalizika jitihada za kuongeza mawakili hao zitakapofanikiwa.
“Tunaomba sekta husika kuliangalia suala hili kwa kutuongezea idadi ya mawakili katika ofisi yetu ili ofisi yetu ifanye kazi zake kwa umakini,” alisema Mzee.
Alisema licha ya uhaba huo wa mawakili, wana mpango wa kuwaendeleza kitaaluma mawakili waliopo ili wawe wabobezi katika kesi maalumu, hatua ambayo alieleza inaweza kuzaa matunda ya kuwa na mawakili weledi kwa kila aina ya kesi. Mkurugenzi huyo alitaja baadhi ya faida ambazo ofisi yake imepata kuwa ni kushiriki kufanya mapitio ya sheria yaliyosababisha utayarishwaji wa miswada ya sheria, ikiwamo sheria ya adhabu ya mwaka 2018 na sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai mwaka 2018.
Faida nyingine ni uendeshaji kesi za udhalilishaji, dawa za kulevya kwa njia ya operesheni na kuamsha ari ya jamii katika kupambana na vitendo vya uhalifu na utoaji elimu kwa umma.
Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar, Jaji Mshibe Bakar alisema tume yao ina jukumu kubwa la kuona sheria zilizopo zinatekelezwa ipasavyo.
Jaji Mshibe aliahidi kusimamia vyema majukumu yao ili kuona kila mmoja anakuwa chini ya sheria.
Naye mkurugenzi Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar, Mussa Haji alisema kila jambo linahitaji umoja na ushirikiano, hivyo kuzitaka taasisi mbalimbali za kisheria kuungana na jitihada za ofisi yake ili kufikia malengo yanayotakiwa na SMZ.
No comments:
Post a Comment