Tuesday, November 21

Mufuruki aipa somo Serikali kuhusu Tanzania ya viwanda


Dar es Salaam. Mwenyekiti wa maofisa watendaji wakuu wa kampuni nchini (CEOrt), Ali Mufuruki ameishauri Serikali kushirikiana kikamilifu na wawekezaji binafsi ili dhana ya Tanzania ya viwanda iweze kufanikiwa.
Mufuruki aliyepata kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), alisema huko nyuma Serikali iliwahi kumiliki viwanda, lakini ikaja kuvibinafsisha kwa wawekezaji.
Aliyasema hayo juzi usiku katika hafla ya uzinduzi wa mwonekano mpya wa gazeti la The Citizen ambalo sasa litakuwa likiangazia zaidi masuala ya kibiashara.
Mufuruki alisema katika ubinafsishaji Serikali zilizopita hazikujikita kuwalea wawekezaji ziliowabinafsishia viwanda, hivyo wakajikuta wakipata matatizo ya uendeshaji kwa kuwa hawakupatiwa malezi mazuri ya uwekezaji.
Alisema kama Serikali inawakaribisha wawekezaji, lakini inashindwa kutoa ushirikiano siku uwekezaji ukiyumba inaweza kulaumiwa.
Alishangaa kuona wawekezaji wakati mwingine wakilaumiwa kwa viwanda hivyo kufa huku Serikali ikiwa haijafanya lolote kutoa sapoti kama kuongezewa mitaji.
Mufuruki aliitaka MCL inayozalisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti kutoogopa kuandika habari zinazozingatia maadili ya taaluma hiyo.
Mufuruki alisema The Citizen inayoonekana leo ni msingi uliojengwa miaka 13 iliyopita kwa kujikita kuandika habari zenye kuzingatia weledi licha ya kuwapo na changamoto kadhaa.
Alisema wakati mwingine wanasiasa wamekuwa hawawaelewi, lakini akaisisitiza menejimenti ya kampuni hiyo kuhakikisha inaitendea haki taaluma ya habari kwa masilahi mapana ya Taifa, huku akidokeza kuwa Serikali na sekta binafsi zinapaswa kufanya kazi kwa ushirikiano.
Akizungumza katika uzinduzi huo, kaimu mkurugezi wa Idara ya Uwekezaji, Aristides Mbwasi aliyemwakilisha waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema Serikali inatambua mchango mkubwa unaofanywa na MCL katika dhana nzima ya Tanzania ya viwanda.
“Tunaishukuru sana MCL kwa kumwalika waziri na leo (jana) angetamani kuwapo ila yupo Dodoma kwa majukumu mengine, tunaipongeza MCL kwa kusaidia kuelimisha wananchi hasa ajenda ya Tanzania ya viwanda katika miaka miwili hii tangu (Serikali ya Awamu ya Tano) ilipoingia madarakani,” alisema Mbwasi.
“Serikali inatambua mchango wenu hasa kuunga kaulimbiu ya Rais John Magufuli ya Tanzania ya viwanda na kama itawezekana ‘products’ (bidhaa) zenu zote hata ile ya Mwanaspoti na Mwananchi muelimishe kuhusu falsafa ya Tanzania ya viwanda.”
Alisema Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wa ndani na nje huku akiwaomba wawekezaji mbalimbali wa kampuni kujitokeza kushiriki maonyesho ya pili ya viwanda yatakayofanyika mwezi ujao katika viwanja vya maonyesho vya Saba saba jijini Dar es Salaam ambapo kiingilio kitakuwa bure.
Mwenyekiti wa Bodi ya MCL, Leonard Mususa alisema kwa sasa kampuni hiyo imeelekeza nguvu katika kuhakikisha inawafikia wananchi kwa njia mbalimbali ikiwamo za kielektroniki.
“Products za MCL ni ‘credible’ (za kuaminika) sio ‘fake’ (bandia), tupo katika ‘print’ na ‘elektronic’ na The Citizen ni gazeti linaloongoza kwa ubora na uzinduzi huu tuwahakikishie wasomaji wetu kwamba tutawafikia kila walipo na kuwapa habari za aina zote,” alisema Mususa.
Akitoa maelezo ya ujio mpya wa The Citizen, mhariri mtendaji mkuu wa MCL, Bakari Machumu alisema kwa sasa asilimia 60 ya gazeti hilo litakuwa na habari za biashara na asilimia 40 ni za matukio ya kila siku.
Awali, mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo, Francis Nanai aliwashukuru wageni waalikwa waliofika katika hafla hiyo iliyofanyika ukumbi wa Hoteli ya Hyatt Kilimanjaro na kuwaomba kuendelea kuunga mkono bidhaa zinazozalishwa na MCL.

No comments:

Post a Comment