Mataifa ya Afrika yameanzisha mkakati kwenye Umoja wa Mataifa, ambao wakosoaji wanasema ni hatua ya dakika za mwisho mwisho ya kuinusuru Burundi kutofanyiwa uchunguzi zaidi juu ya madai ya uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Septemba 25, tume hiyo ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa ilitoa mwito kwa mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC kuchunguza visa vya uhalifu dhidi ya ubinaadamu nchini Burundi. Matukio kama mauaji, utesaji, unyanyasaji wa kingono, utoroshwaji kwa nguvu na kukamwata ovyo, yamekuwa yakiendelea kutokea tangu Aprili 2015, baada ya Rais Pierre Nkrunziza kuingia madarakani kwa awamu ya tatu, hii ikiwa ni kulingana na ripoti iliyotolewa mapema mwezi huu.
Baraza la haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa lilikuwa likitarajiwa kuunga mkono azimio la Umoja wa Ulaya leo hii la kuongeza mamlaka ya tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa ambayo ilisema viongozi wa juu wa Burundi wanapaswa kuwajibika kwa uovu nchini humo.
Lakini kundi hilo la mataifa kutoka Afrika, linaloongozwa na Tunisia, liliitisha mkutano wake jana Jumatano na kuweka wazi azimio tofauti, ambalo liliisifu Burundi kwa kuonyesha nia ya kufanyika kwa mazungumzo na kushirikiana na Umoja wa Mataifa, bila ya kuzungumzia lolote kuhusu kuanzishwa upya kwa uchunguzi.
Balozi wa Burundi Renovat Tabu alidai kwamba tume hiyo ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa ilikuwa na upendeleo na ripoti zake kuhusu machafuko na uovu hazikuakisi uhalisia.
Tume yataka ICC kuingia kati iwapo Burundi haitarekebisha mfumo wa kisheria.
Kwenye mkutano wa tume hiyo ya uchunguzi uliofanyika Jumatatu mjini Brussels, rais wake Fatsah Ouguergouz, alisema iwapo serikali ya Burundi haitaweza kuzungumzia uhalifu, basi suala hilo litatakiwa kukabidhiwa kwa taasisi nyingine. Na taasisi pekee inayoweza kufanya kazi hiyo ni ICC.
Mabalozi kutoka Umoja wa Ulaya, Marekani, Norway, Uswisi, Canada na Uingereza walikataa kujadili maudhui ya azimio la kundi hilo la mataifa ya Afrika na kueleza kukasirishwa huku kukisalia saa 24 tu kabla baraza kuanza kufanya maamuzi juu ya maazimio ya Umoja huo wakati kikao kilichodumu kwa wiki tatu kinapomalizika.
Wawakilishi wa Umoja wa Ulaya walisema hali nchini Burundi bado ni tete na kuna uwezekano wa kuendelea kutokea kwa visa vya kutisha vya uvunjwaji wa haki za binaadamu.
Mwakilishi wa Marekani alisema hatua ya ghafla ya Burundi ya kutaka kushirikiana, wakati hapo awali iligoma kufanya kazi na tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa, ilionekana kuanza si zaidi ya siku tatu zilizopita. "Nadhani mazungumzo haya yataendelea, lakini kwa upande mwingine sidhani kama tunaweza kukubali ushahidi wa chini ya asilimia moja ya mwaka kuakisi kile kinachoweza kutokea," aliuambia mkutano.
Mkakati huo wa kundi la mataifa ya Afrika kuchukua jukumu la kuichunguza Burundi unaakisi mwendelezo wa mwenendo wa viongozi wa Afrika wa kukwepa masuala mazito kutoka Umoja wa Mataifa, na hususan mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC ya mjini The Hague.
No comments:
Post a Comment