Thursday, October 5

Familia ya Tundu Lissu wataka upelelezi wa kimataifa kuingia kati

Ndugu zake Tundu Lissu, Vincent Mughwai(kushoto) na Alute Mughwa (kulia)
Image captionNdugu zake Tundu Lissu, Vincent Mughwai(kushoto) na Alute Mughwa (kulia)
Familia ya mnadhimu mkuu wa kambi ya upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu, imeiomba serikali ya nchi hiyo kuongeza kasi ya upelelezi wa kesi ya kushambuliwa kwa mbunge huyo wa Singida mashariki aliyepigwa risasi mnamo mwanzoni mwa mwezi jana huko mjini Dodoma.
Familia hiyo iliyowakilishwa na kaka zake wawili, wameitaka serikali kuvishirikisha vyombo vya upelelezi vya kimataifa kama vinavyoshirikishwa katika mambo mengine ili kuongeza ufanisi katika upelelezi huo.Tundu Lissu alipigwa risasi zaidi ya thelathini na watu ambao mpaka sasa hawafahamiki pindi alipokuwa mjini Dodoma akihudhuria vikao vya bunge.
Kwa upande wake, katika siku za hivi karibuni, jeshi la polisi nchini Tanzania lilisema upelelezi wa tukio hilo unasuasua kutokana na dereva wa Mbunge huyo kutofika polisi kutoa ushahidi.Hata hivyo, taarifa kutoka Chadema zinasema kuwa dereva wa mbunge huyo yuko nchini Kenya kwa ajili ya kupata matibabu ya kisaikolojia kutokana msongo wa mawazo alioupata baada ya kisa hicho.
Kufuatia kauli hiyo, familia hiyo imeliomba jeshi la polisi kufanya utaratibu wa kumfuata dereva huyo mjini Nairobi kwa ajili ya mahojiano ili uchunguzi uendelee.
Tundu Lissu yuko nchini Kenya kwa takribani wiki nne sasa ambako anapatiwa matibabu kutokana na majeraha ya risasi aliyoyapata kutokana na shambulio hilo.

No comments:

Post a Comment