Kiongozi wa Korea Kaskazini amepokezwa habari kuhusu mpango wa taifa hilo wa kutaka kurusha kombora hadi katika kisiwa cha eneo la pacific cha Guam kinachomilikiwa na Marekani kulingana na ripoti za vyombo vya habari.
Lakini ripoti hiyo imesema kuwa itachunguza vitendo vya Marekani kabla ya kuchukua hatua ya kurusha kombora hilo katika kisiwa cha Guam.
Wiki iliopita, Korea Kaskazini ilionya kwamba mikakati inawekwa kushambulia eneo ambalo ndege za kijeshi za Marekani zimekita kambi.
Kumekuwa na cheche za maneno kati ya Marekani na Korea kaskazini.
Ripoti hiyo ya kitengo cha habari cha KCNA ilisema kuwa Kim Jong un aliutazama mpango huo kwa muda mrefu na kuujadili na maafisa wakuu wa jeshi.
Kamanda wa jeshi la kimkakati la Korea Kaskazini sasa anasubiri agizo baada ya kuandaa shambulio hilo la Guam.
Lakini ripoti hiyo pia imeongezea kwamba kiongozi wa Korea Kaskazini atachunguza mienendo ya Marekani kabla ya kutoa uamuzi wowote, hatua inayoonekana kupunguza kasi ya cheche za maeneo kati ya mataifa hayo mawili.
Mwandishi wa BBC Yogita Limaye mjini Seoul anasema kuwa hatua hiyo itapunguza wasiwasi na kuzuia mgogoro wa kijeshi katika eneo la Korea.
Mwandishi mwengine ameongeza kuwa baada ya siku kadhaa za vitisho kutoka Pyongyang ,inaonekana kwamba rais Kim Jong Un sasa anataka kunyamaza na kutazama hali ,lakini katika taifa lenye siri kubwa kama Korea Kaskazini huwezi kuwa na hakika.
Wachanganuzi wanasema inamaanisha kwamba Pyongyang haiko tayari kutekeleza shambulio katika kisiwa cha Guam, kwa hivyo huenda inachukua muda.
Hatua hiyo inajiri baada ya waziri wa ulinzi nchini Marekani James Mattis kuonya kwamba shambulio lolote linaweza kusababisha vita vikali, na iwapo Pyongyang itarusha kombora kuelekea Guam basi ''itakuwa vita''.
Ameambia maripota kwamba Jeshi la Marekani litatetea taifa hilo kutoka kwa shambulio lolote wakati wowote na kutoka kwa taifa lolote.
Pia aliwahakikisha raia wa Guam ,ambapo kuna kambi za kijeshi za Marekani kwamba takriban watu 160,000 wanalindwa na akasema iwapo kombora litarushwa ''tutalitibua''.
No comments:
Post a Comment