Zanzibar: Chama cha Mapinduzi (CCM) visiwani hapa jana kilifanya mkutano na waandishi wa habari kwa ajili ya kutoa tamko la kurasa nane kuzungumzia msimamo wake dhidi ya uamuzi wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kujivua uanachama, kikisema kuwa hakipo pamoja naye.
Lowassa, ambaye uamuzi wake wa kuhamia Chadema mapema wiki hii umeongeza ushindani katika mbio za urais, alijivua uanachama wa CCM akisema mchakato wa kumpata mgombea wa urais kwa tiketi ya chama hicho ulikiuka katiba na kanuni.
Uamuzi wa mbunge huyo wa Monduli kuhamia upinzani na kitendo cha CCM kuengua jina lake umefuatiwa na wabunge, madiwani na wanachama kadhaa kutangaza kujivua uanachama na kujiunga na vyama vya upinzani, hasa Chadema.
Uamuzi wa mbunge huyo wa Monduli kuhamia upinzani na kitendo cha CCM kuengua jina lake umefuatiwa na wabunge, madiwani na wanachama kadhaa kutangaza kujivua uanachama na kujiunga na vyama vya upinzani, hasa Chadema.
Lowassa hakuwahi kusema kuwa uamuzi wake unaungwa mkono na CCM Zanzibar.
Lakini jana, uongozi wa chama hicho mjini hapa uliitisha mkutano na waandishi wa habari kueleza kuwa hakimo katika wimbi hilo la kumfuata Lowassa kwenda upinzani.
Wakizungumza katika mkutano huo uliofanyika ofisi za makao makuu ya CCM mjini hapa na kurushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha Shirika la Utangazaji Zanzibar pamoja na kituo cha TBC1 cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), viongozi hao walitetea utaratibu uliotumika kuengua jina lake wakisema ulikuwa sahihi.
“Sisi kama wana-CCM na maelfu ya wanachama wengine hatukubaliani naye,” alisema katibu wa Mkoa wa Mjini, Mohammed Omar Nyawenga wakati akisoma tamko hilo katika mkutano huo uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama cha Serikali, akiwamo Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho na mjumbe wa Kamati Kuu, Shamsi Vuai Nahodha.
“Wana-CCM waliomuunga mkono Lowassa hasa kutoka mikoa mitano ya Zanzibar walimuunga kwa kuamini kwamba yeye ni kiongozi ambaye amepitia katika uozefu mkubwa katika chama chake, lakini hawakumuunga mkono kwa sababu ya sura yake wala utajiri wake. Hapana.
“Bali ni kwa sababu ya siasa, sera na ilani za chama alichokiamini na kukipigania, yaani CCM hivyo kwa kuwa sasa ameamua kujitenga na CCM basi nasi tumeamua kujitenga naye na kamwe hatupo pamoja naye.”
Alisema maelfu ya wana-CCM wa Zanzibar walimuunga mkono kutokana na azma yake ya kuomba kuteuliwa na CCM kuwa mgombea wake wa kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini kutokana na kubadilika kwake wamemuachia mkono.
Alisema CCM ni muumini wa haki za binaadamu, usawa, wa sheria hivyo kujiondoa Lowassa ni sawa na ilivyokuwa wakati wa kujiunga kwake .
“Ni suala la hiyari yake na wala hatuna ugomvi naye. Ila tunamkumbusha tu kwamba inawezekana kabisa umaarufu alionao sasa umejengwa kutokana na CCM, lakini haiwezekani kabisa kuwa maarufu wa CCM umejengwa na au umetokana na yeye. Ndio maana tunasema chama kwanza, mtu baadaye,” alisema katibu huyo.
Nyawenga alisema CCM, yenye viongozi wenye hekima, busara, mapenzi na uadilifu mkubwa kwa wananchi, bado inaaminiwa na kukubalika miongoni mwa wananchi wengi wa Tanzania.
Alisema wingi huo wa wanachama wake hautokani na wala haujaletwa na utajiri wa viongozi wake bali unatokana na uimara wa siasa, sera na itikadi yake.
“Hasara ya kweli kwa CCM si kumpoteza tajiri mmoja anayetaka kubadili sera na itikadi ya CCM kwa maslahi yake binafsi na marafiki zake bali ni kuwapoteza mamilioni ya wanachama wake ambao wanachoshwa na viongozi walafi na wanafiki ndani ya CCM,” alisema.
Alisema kwa kuzingatia ukweli huo, uamuzi wa Lowassa kujiondoa ndani ya CCM si jambo la kukishitua chama hicho, viongozi wake wala wanachama wake kwani CCM kamwe haiwezi kudhoofika wala kupasuka.
“Hii si mara ya kwanza kwa CCM kuondokewa na kiongozi mwandamizi na kujiunga na upinzani. Mwaka 1989 CCM iliwafukuza uanachama jumla ya viongozi waandamizi 11 akiwemo waziri kiongozi wa zamani Maalim Seif Sharif Hamad akifuatiwa na Augustine Mrema ambaye alijiunga na NCCR Mageuzi,” alisema.
Pia alisema mwaka 2014, CCM ilimfukuza mwakilishi wake na mweka hazina wa chama hicho, Mansoor Yussuf Himid na haijapoteza kitu kutokana na kitendo hicho.
“Kama mvuvi wa pweza tutakutana mwambani,” alisema.
Aliwashangaa viongozi wa upinzani hasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), hususan viongozi wa Chadema kwa namna wanavyoendesha siasa alizoziita za ubabaishaji na ulaghai kwa Watanzania hata baada ya nchi kufikisha miaka 23 tangu kurejeshwa kwa siasa za ushindani.
Alisena tangu mwaka 1992, vyama vya upinzani vimeshindwa kuandaa wagombea wenye uwezo wa kuwaongoza Watanzania na kuishia kudaka mapumba yanayotoka CCM.
“Mara nyingi tumewasikia wakijitoa kimasomaso kwa kukariri nusu nusu maneno ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere yanayosema ‘Watanzania wanahitaji mabadiliko na wasipoyapata ndani ya CCM, watayapata nje ya CCM’,” alisema.
“Kwa bahati mbaya sana wasia huu wa Baba wa Taifa unakaririwa nusu nusu. Naomba niwakumbushe viongozi wa Ukawa wasia huo unaendelea kutamka kwamba Rais wa Tanzania anaweza kutoka chama chochote kile lakini Rais bora wa nchi yetu atatoka CCM.”
Borafya Silima
Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Mjini, Borafya Silima ambaye alikuwa kinara wa kampeni za Lowassa na aliyewahi kutangaza kwamba anawakilisha wenyeviti wote wa mikoa mitano ya Zanzibar kumuunga mkono waziri huyo mkuu wa zamani, alisema wameachana na Lowassa kwa madai kuwa anataka madaraka zaidi.
Borafya, ambaye aliitisha mkutano huo wa jana na ambaye aliuongoza, alikiri kuwa walimpendekeza Lowassa kwa kuwa amefanya kazi nzuri katika chama, lakini wameachana naye baada ya kuona amekuwa anataka zaidi madaraka kama Maalim Seif.
Borafya alianza kubabaika wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari akitumia muda mwingi kujitetea na kumrushia lawama Maalim Seif Sharrif Hamad badala ya kujibu maswali.
“Kuna ishara kwamba labda huyu mtu anapenda ukubwa na madaraka kama Maalim Seif. Sisi chama chetu unatakiwa ukiambiwa nenda huku unaende, ukiambiwa fanya hivi, fanya” alisema Borafya.
“Chama chetu hakitaki mtu anayependa madaraka mkubwa kama Lowassa na kama Maalim Seif, mtu huyu anapenda madaraka makubwa sidhani kama wanachama wa CCM watamfuata Lowassa,” alisema Borafya.
Borafya alisema alikuwa mtu wa kwanza kumuunga mkono Lowassa kwa sababu chama chake kilimteua na alifanya hivyo kwa dhati ya roho yake na mapenzi yake kwa Lowassa na ndio maana kila anapopita alimpigia debe akisema kwamba yeye ana mahaba naye.
Kuhusu tuhuma za rushwa dhidi ya Lowassa, alisema CCM haijawahi kumuhusisha mbunge huyo wa Monduli na suala hilo, bali upinzani.
Nahodha akana mizengwe
Wakati Borafya akitetea uamuzi wake wa awali wa kumpigia debe Lowassa, mjumbe wa Halmshauri Kuu wa CCM Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha alitumia muda mwingi kutetea utaratibu uliotumika kumpata mgombea wa urais wa chama hicho.
“Kazi ya Kamati Kuu si kuwaondoa wagombea bali ni kujadili wagombea kama walivyofanya mwaka 2005,” alisema na kutaja majina ya makada waliopitishwa mwaka huo kuwa ni Jakaya Kikwete, Salim Ahmed Salim, Frederick Sumaye, Abdallah Kigoda na Mark Mwandosya.
“Lowassa alikubaliana na utaratibu huo bila ya kuukosoa kwa kuwa ulikidhi haja na matakwa yake,” alisema Nahodha.
“Utaratibu huohuo ndio uliotumika mwaka huu wa kuwateua wagombea, lakini jambo la kushangaza ni kwamba kuna watu wanasema taratibu zimekiukwa wakati hakuna kilichobadilika.
“Utaratibu wetu sisi ni kuwajadili watu kwa sifa na mtu akiwa na sifa za msingi anateuliwa, lakini hizo hoja za kuwa mwenyekiti amekuja na majina yake mfukoni, ni hoja zisizo na msingi na ni hoja za kipuuzi.
“Mimi inanisikitisha sana nikisikia mtu anasema taratibu zimekiukwa kwa sababu tu matakwa yake hayajatimizwa. Mimi kama mtu wa kulalamika, basi angesema Dk (Mohamed Gharib) Bilal kwa sababu yeye ni mtu wa pili baada ya Rais, lakini hatujamsikia kulalamika wala kusema lolote.”
Alisema CCM imefuata utaratibu uliopo ingawa wapo wanachama ambao wanataka utaratibu unaotumika hivi sasa ubadilike kulingana na wakati uliopo, lakini akasema hayo yatajadiliwa kwa wakati wake.
Nahodha alisema wapinzani waliomkumbatia Lowassa ndio waliokuwa wakimtuhumu Lowassa kwa kula rushwa na si kiongozi yeyote wa chama cha CCM wala si serikali.
Alisema kwamba tatizo kubwa kwamba watu hawataki kukosolewa wala kuelezwa ukweli hivyo kama kuna watu wanaamini
“Yule ambaye alimfuata Lowassa leo hayupo CCM na hatarudi tena, lakini yule ambaye alimfuata Lowassa kwa sababu aliamini huyu ni kada wa CCM na kila anachokifanya anafanya kwa CCM, basi CCM ipo na itadumu milele,” alisema Nahodha huku akishangiliwa.
Nahodha alisema sifa za mgombea wa urais wa CCM zinaeleweka na kwamba Dk John Pombe Magufuli aliyeteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho ana sifa zote.
Ramadhan Abdallah Shaaban
Waziri wa Maji Nishati na Ardhi, Ramadhan Abdallah Shaaban alisema katika kumteua mgombea kunafuatwa sheria na kanuni na kumtafuta mgombea kunatakiwa kumteua mtu asiye na shaka, lakini Lowassa alikuwa ametiliwa na shaka.
“Wapinzani wao ndio walikuwa wamemtilia shaka kwa hivyo sisi CCM tumeona huyu ameshatiliwa shaka kwa hivyo ndio maana tukamkataa,” alisema Shaaban.
Ramadhan alisema Lowassa alitendewa haki kikamilifu na suala la kwamba kuna watu walimuunga mkono baadaye wakakataa kumuunga mkono ni kwa sababu ya yaliyotokea ndani ya kikao cha Kamati ya Maadili.
“Unaweza kumuunga mkono mtu lakini ukasikia baadaye ana mambo yake, ukakataa kumuunga mkono…na Rais (wa awamu ya tatu, Benjamin) Mkapa aliwahi kusema kuwa ukikaa pale kwenye kiti unayajua mambo mengi kwa hivyo nasema Kamati Kuu haikukosea kumuengua Lowassa. Funika kombe mwanaharamu apite,” alisema Ramadhan.
Haji Omar Kheri
Kada mwingine aliyeweka msimamo wake kuhusu Lowassa kwenye mkutano huo ambao ukikatishwa mara kwa mara kwa vicheko na nyimbo, alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Vikosi Maalumu), Haji Omar Kheri ambaye alisema hakuna haja ya kumnyang’anya kadi ya CCM mgombea huyo wa urais wa Chadema, na badala yake wanafuta jina lake kwenye daftari la wanachama.
No comments:
Post a Comment