Meneja wa Kikosi cha Ujenzi wa TBA, Humphrey Killo alisema jana kuwa uvunjaji wa ofisi na ukumbi ulifanyika usiku wa kuamkia juzi ikiwa ni maandalizi ya kuvunja sehemu ya jengo la ghorofa 10 lililoko eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam ambalo liko kwenye hifadhi ya Barabara ya Morogoro.
Ubomoaji huo unafanyika pia ili kupisha utekelezaji wa mradi wa barabara za juu eneo la Ubungo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli.
Novemba 15, Rais Magufuli aliagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuweka alama za X kwenye jengo hilo katika sehemu zilizo katika hifadhi za barabara.
Akizungumzia uvunjaji wa jengo hilo, Killo alisema kwa sasa wanafanya maandalizi yakiwemo ya vifaa kama vile mitambo na malori ya kubebea vifusi. “Maandalizi haya ni pamoja na kubomoa majengo madogo kama vile ofisi za walinzi na ukumbi wa mikutano na sehemu ya mapokezi,” alisema Killo aliyekuwa akisimamia mchakato huo.
Killo alisema maandalizi yanatarajiwa kukamilika kesho na utaratibu utakaofuata ni kubomoa jengo la ghorofa akisema kazi hiyo inaweza kufanyika kwa mwezi mmoja.
Alisema kabla ya kubomolewa ghorofa hilo, jengo lote litawekwa vyuma na kuzungushiwa nyavu maalumu ili kuzuia vumbi kusambaa katika maeneo mengine ya jirani.
“Nyavu hizi zitasaidia pia kuzuia vitu au vipande vidogovidogo vitakavyokuwa vikitoka wakati wa ubomoaji,” alisema Killo.
Alisema ubomoaji ni hatari hivyo timu ya wataalamu 10 wa fani mbalimbali wakiwamo wasanifu wa majengo watapelekwa kusimamia kazi hiyo itakapoanza.
“Wataalamu wengine watakuwa ni wa fani ya uhandisi wa majengo, wakadiriaji wa majenzi na mafundi sanifu. Pia, watakuwepo maofisa usalama kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na usalama,” alisema Killo.
Alisema jengo hilo lina sehemu tatu; ya mbele, katikati na nyuma hivyo ubomoaji utahusisha sehemu ya mbele pekee.
Novemba 27, uongozi wa Tanesco ulitoa taarifa kwa umma ukisema utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli umeanza kuhusu kubomolewa jengo.
Kaimu Meneja Uhusiano wa Tanesco, Leila Muhaji, Novemba 28 alisema wafanyakazi wa shirika hilo wamehamia ofisi zingine za shirika hilo zilizoko jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment