Monday, December 4

UTARATIBU UNAOSTAHILI KUFUATWA KABLA YA KUFUTIWA UMILIKI WA ARDHI.

Image result for HATI MILIKI
NA  BASHIR  YAKUB -

Yafaa  kujua  utaratibu unaotakiwa  kufuatwa  kabla  ya kufutiwa  hati miliki  ya  ardhi (nyumba/kiwanja).  Unapojua utaratibu  huu  ndipo  unapojua kama  ulionewa  au  hapana. Na kuonewa ni  pamoja na  kukiuka utaratibu.  Na  kukiuka  taratibu yoyote  ya  kisheria kunabatilisha  mchakato wa  kufutwa  kwa  hati yako na  kutakiwa  kurudishiwa  eneo  lako  au  fidia.

Makala  yaliyopita  tulieleza mambo  ambayo  ukifanya  unahesabika  kukiuka  masharti  ya  umiliki wa  ardhi   na ni hapo  unapoweza   kufutiwa  umiliki. Leo  tuangalie  utaratibu  wa  kufuta umiliki  ikiwa imethibitika  kuwa   tayari  umekiuka  masharti  hayo. Sheria  namba 4 ya 1999 , Sheria  Ya  ardhi  imeeleza  utaratibu  wa  kufuta  umiliki  wa  ardhi.

 UTARATIBU.

1.Ni  lazima  uwe umekiuka  masharti  au  moja  ya  masharti uliyopewa  wakati unakabidhiwa  ardhi/hati kwa  mujibu  wa  kifungu  cha 48 ( 1) cha  Sheria  ya  ardhi. Usikubali  kufutiwa  umiliki  ikiwa  hujakiuka  sharti/masharti ya umiliki uliyopewa,  labda   iwe  vinginevyo.

2.   Baada  ya  kuwa  umekiuka  masharti  yafaa  upewe  taarifa  maalum( notice) kwa  mujibu  wa  kifungu 48(2). Ni  taarifa inayoeleza  masharti  ya  umiliki  uliyokiuka  na  onyo  la  kufutiwa  umiliki.  Taarifa  hiyo  ni  ya  siku  90(miezi  mitatu).  Taarifa  hiyo utapewa wewe  mmiliki  na  kila  mwenye  maslahi  katika  ardhi  hiyo  mf, mpangaji, mrehani nk.

3.   Baada  ya  siku 90  kuisha na  pengine  hujajirekebisha  au  kufanya  kile  ulichoambiwa  kufanya  basi  kamishna  wa  ardhi  atatakiwa  kupeleka  pendekezo  kwa  rais  ili  kufutiwa umiliki. Ni  rais  tu  mwenye  mamlaka  ya  kufuta  umiliki  wa  ardhi. 

Zingatia, barua  au  nyaraka  nyingine yoyote  ambayo inasema  umefutiwa  umiliki  lakini  aliyefuta  sio  rais  wa  nchi,  sio  halali.

4.  Ikiwa rais  atakubali  kukufutia  umiliki  wa  ardhi basi  inatakiwa kufutwa  huko  kutangazwe  katika  gazeti  maalum  la  serikali/taarifa ya  serikali(GN)  na  katika  gazeti  la  kawaida(newspaper)  ambalo  linafika  eneo  ardhi  yako  ilipo.  Hii  ni  kwa  mujibu  wa  kifungu  cha 49(1).  Ili  utaratibu  uhesabike  umefuatwa  ni  lazima  matangazo  haya  yatolewe  la  sivyo  kufutiwa  huko  kunabatilika.

5.  Rais  atakapofuta  umiliki  wa  ardhi basi  ardhi  hiyo  itahama  kutoka  kwa  mmiliki  wa  awali  kwenda  serikalini  au  vinginevyo itakavyoamriwa kwa  mujibu  wa  kifungu cha 49(2).  

6. Ikiwa  kuna  maendelezo  yoyote  ya  kudumu  ambayo  ulifanya  kwenye  hiyo  ardhi  basi   ni  lazima  ulipwe  fidia  ya  maendelezo  hayo  kwa  mujibu  wa  kifungu  cha  49(3). 

Isipokuwa maendelezo  hayo  yawe  yalikuwa  ni sehemu  ya  masharti  ya  umiliki  wa  ardhi  hiyo.  Yasiwe  nje  ya  yale  uliyokuwa  umepewa kwenye umiliki.

7. Ikiwa   ardhi  hiyo  ilikuwa  inadaiwa  kodi au tozo  za ardhi basi  kodi  na  tozo  hizo  zinaondolewa  na  deni  hilo  linakufa, mpaka  isemwe  vinginevyo.  Hii  ni  kwa  mujibu  wa  kifungu cha 49(2)(e)..

NAMNA  YA  KUDAI  HAKI  YAKO  IKIWA  TARATIBU  ZIMEKIUKWA.

Kwanza, waweza  kupeleka  malalamiko  yako  kwa  kamishna  wa  ardhi    na  baadae  kwa  rais. Utaandika  barua  ikieleza kile  ambacho  unahisi  kuonewa au  taratibu  kukiukwa.

Pili, ni  kupeleka  malalamiko  yako  mahakamani. Hapo  sio barua  bali utapeleka  nyaraka  maalum  za  kufungulia  shauri(Plaint/Application). Humo  pia  utaeleza  pahala  unapohisi  kuonewa au  taratibu  kukiukwa pia.
Pia  unaqweza  kuchukua  hatua  hizi  kwa  pmoja na  kwas  wakati moja.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI   KILA   JUMANNE.  0784482959,  0714047241bashiryakub@ymail.com

No comments:

Post a Comment