Kenya imesema kwamba itaendelea na mpango wake wa kuhakikisha kwamba ina kiwanda cha kuzaliwa umeme kwa kutumia nguvu za nyuklia kufikia 2027.
Afisa Mkuu Mtendaji wa Bodi ya Umeme wa Nyuklia ya Kenya Collins Juma ameambia mkutano wa wadau kuhusu kawi jijini Nairobi kwamba ujezi wa kiwanda cha kuzalisha kawi hiyo unatarajiwa kuanza 2024.
Bodi hiyo imesema nishati hiyo itatumiwa kuongeza uzalishaji wa umeme nchini humo na si kuchukua nafasi ambayo imekuwa ikitekelezwa na vyanzo vingine vya kawi nchini humo.
Kufikia mwaka 2030, ambapo Kenya inatazamia kuwa taifa lenye viwanda la mapato ya wastani kufikia wakati huo, Kenya itakuwa ikihitaji megawati 17,000.
Kawi ya mvuke itachangia megawati 7,000. Kwa sasa, kawi hiyo kwa sasa hutumiwa kuzaliwa megawati 2,400 za umeme nchini humo.
Kaimu afisa mkuu mtendaji wa kukinga dhidi ya miali nururishi nchini Kenya Joseph Maina amesema Wakenya hawafai kuwa na wasiwasi kuhusu usalama wa nishati ya nyuklia.
"Kumekuwa na ajali tatu pekee kubwa za nyuklia katika historia. Kisiwa cha Three Mile Marekani, 1978; Chenorbyl nchini Ukraine, 1986 na Fukushima nchini, Japan, 2011. Usalama umeimarishwa kutokana na mafunzo kutoka kwa mikasa hiyo," amesema.
Kenya imekuwa na mpango wa kuzalisha kawi ya nyuklia kwa muda.
Machi mwaka huu, Waziri wa nishati na mafuta wa nchi hiyo Bw. Charles Keter alisema Kenya itatimiza vigezo vikali vilivyowekwa na Shirika la kimataifa la nishati ya atomiki IAEA kabla ya kutekeleza mpango huo.
Alikadiria kwamba Kenya itatumia dola 5 bilioni za Marekani kujenga kiwanda cha kuzalisha kawi hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti ya IAEA ya mwaka 2015, zaidi ya nchi 30 duniani, theluthi moja zikitoka Afrika zinajiandaa kuanzisha mipango ya nyuklia kwa ajili ya kuzalisha umeme kwa usaidizi wa wataalamu kutoka shirika hilo.
No comments:
Post a Comment