Monday, December 4

RC: Mwanafunzi aliyeuawa alitaka kuwa rubani


Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amesema Humphrey Makundi, mwanafunzi aliyeuawa na kuzikwa katika mazingira ya kutatanisha, alitamani siku moja kuwa rubani, lakini ameondoshwa duniani kutokana na roho ya ukatili.
“Huu ni ukatili dhidi ya watoto na ni pengo kwa Taifa. Ni pengo kwa mkoa na pengo kwa Jimbo la Vunjo kutokana na mtoto huyu kuwa na ndoto kubwa kwa Taifa hili,” alisema Mghwira juzi katika ibada ya mazishi ya mtoto huyo aliyekuwa mwanafunzi wa Sekondari ya Scholastica ya mjini Himo.
“Nimepata taarifa kuwa alikuwa na ndoto ya kuwa rubani, haki itendeke na uvumilivu unahitajika zaidi hasa kipindi hiki kigumu cha kumpoteza Humphrey.”
Mwili wa mwanafunzi huyo aliyetoweka shuleni uliokotwa Mto Ghona, Novemba 10 na kuzikwa Novemba 12 na Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, lakini ulifukuliwa kwa amri ya mahakama kwa ajili ya vipimo vya vinasaba (DNA).
Pia, mkuu huyo wa mkoa alieleza kusikitishwa na kutokuwapo mwanafunzi hata mmoja kutoka shule hiyo au mwalimu katika kuaga mwili wa Humphrey.
Alisema baadhi ya wananchi mkoani Kilimanjaro wamejawa na roho za kikatili, udhalimu na rushwa, mambo ambayo yanatakiwa kukomeshwa haraka.
Mkuu huyo wa mkoa alisema licha ya kwamba hakuna mtu aliyekamatwa, lakini ofisi yake imepata malalamiko mengi kuhusu vitendo vya rushwa vinavyoendelea mahakamani.
Mghwira aliyeongozana na kamanda wa polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah katiba ibada hiyo alisema Humphrey amepumzika, hivyo ni vyema wakaiachia mahakama ili haki itendeke.
Katika mahubiri kwenye ibada hiyo, mchungaji Samwel Mshana wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) alikemea vitendo vya kishirikina.
Mchungaji huyo aliiomba familia na jamii kutolipiza kisasi, badala yake wawasamehe wote na kushirikiana kupiga vita vitendo vya ukatili na ushirikina.
Alisema Mkoa wa Kilimanjaro ni miongoni mwa ile ambayo inasifika kwa amani, lakini katika miezi ya karibuni vitendo vya kikatili vimeanza kuongezeka.
Katika salamu zake kwa wananchi, mbunge wa Vunjo, James Mbatia alisema damu inayomwagika itawalaani waliohusika na kuwataka watu kuacha kujihusisha na ukatili.
Alisema sababu inayosababisha kumwaga damu kwa walio wengi ni jeuri, kiburi na kujiona wana mali jambo linalosababisha haki ya wanyonge na damu yao kupotea.
“Haki ni haki hata kama itadhulumiwa lakini ipo siku moja itapatikana. Ninawaomba viongozi wa kiroho kuendelea kuhubiri amani na upatanisho,” alisema Mbatia.
Mbunge huyo alisema damu ya Mtanzania mmoja ikimwagika humrudia Mwenyezi Mungu.
Pia, alimuomba Rais John Magufuli kuliangalia suala la umwagaji damu linalotokea katika maeneo mbalimbali nchini ili sheria ichukue mkondo wake.
Hivi karibuni mmiliki wa Sekondari ya Scolastica iliyopo mji wa Himo, Edward Shayo (63); mlinzi Hamis Chacha (28) na makamu mkuu wa shule hiyo, Laban Nabiswa (37) walifikishwa mahakamani wakituhumiwa kuhusika na kifo cha Humphrey.
Washtakiwa hao walifikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi na kusomewa shtaka la kuua kwa kukusudia.
Akiwasomea shtaka hilo Novemba 27, Wakili wa Serikali, Kassin Nassir alidai walitenda kosa hilo Novemba 11. Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za mauaji.
Baada ya kusomewa shtaka hilo walipelekwa rumande na kesi dhidi yao itatajwa Desemba 8.

No comments:

Post a Comment