WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi ambaye pia ni Mbunge wa Ismani, ameivunja nyumba yake iliyopo Mapogoro, Ismani kama njia ya kumuunga mkono Rais John Magufuli katika ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kati ya Iringa kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Akizungumza jana mara baada ya kushiriki zoezi la ubomoaji wa nyumba hiyo, Waziri Lukuvi, alisema kuwa akiwa kama kiongozi ameamua kuwa wa kwanza kuonyesha mfano kwa kuanza kuivunja nyumba hiyo ambayo kimsingi sehemu ya robo ilikuwa imepigwa alama ya X nyekundu na robo tatu ilipigwa alama ya X ya kijani, ila kutokana na kuunga mkono jitihada za Serikali katika ujenzi wa barabara hiyo, ameamua kuivunja yote na hatadai malipo yoyote.
“Kimsingi barabara hii ya kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, ilianza kabla ya sisi kuja kujenga hivyo barabara tuliikuta hakuna hata mmoja kati yetu ambaye barabara ilimkuta na haya ni maendeleo yetu sote na Taifa kwa ujumla, mimi nilijenga jirani na barabara ili kuwapungia watu mikono wakati wanapita sikujua kama ni barabarani, ila baada ya kujulishwa nimeamua kwa mikono yangu kuja kuvunja nyumba yangu.”
Waziri Lukuvi alisema Serikali haitalipa fidia yoyote kwa wananchi waliojenga nyumba katika hifadhi ya barabara akiwamo yeye mwenyewe, hivyo alitaka wananchi wote ambao walivunja sheria kwa kutojua waanze kuvunja nyumba zao wenyewe kwa hiari bila kusubiri kuvunjiwa.
Alisema kuwa wananchi wote waliowekewa alama ya X katika nyumba zao, kuanza kuvunja pasipo kusubiri kujiuliza na maana ya alama nyekundu ama kijani, kwani barabara hiyo ilianza toka miaka 30 hivyo hifadhi ya Ruaha na barabara hiyo ilianza kabla ya hapo.
No comments:
Post a Comment