Friday, November 10

Nape asema miradi ya Serikali inaongeza deni la taifa


Dodoma. Mijadala imetawala bungeni  leo huku Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye akisema miradi mikubwa itakayotekelezwa na Serikali, itafanya deni la taifa kufikia Trilioni 47.
Mbali na Nape ambaye mchango wake umeonekana  kuwa mwiba kwa Serikali, lakini wabunge kutoka Zanzibar wamechachamaa kutokana na mpango wa maendeleo wa taifa kutoihusisha Zanzibar.
Katika mijadala hiyo, Waziri wa zamani wa Fedha, Saada Mkuya,  ameenda mbali na kumtuhumu waziri wa sasa wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango kutofanya kikao cha kazi Zanzibar tangu ateuliwe.
Hayo yalijitokeza wakati wabunge wakichangia mapendekezo ya Mpango wa maendeleo wa Taifa na mwongozo wa kuandaa bajeti kwa mwaka wa fedha 2018/2019 uliowasilisha bungeni na, Dk.Mpango.
Akichangia taarifa hiyo kwa hisia, Nape amesema  binafsi hapingi kutekelezwa kwa miradi mikubwa ila anapingana na Serikali jinsi ya kuifadhili na kuiendesha kwa kutumia fedha za Serikali.
“Niliposoma nilishtuka kidogo kuona Serikali inapendekeza kuwekeza pesa za Serikali kwenye miradi ambayo inaweza kuendeshwa kibiashara. Nilitegemea miradi hii tungeruhusu sekta binafsi,” amesema.
Ametaja baadhi ya miradi ya ambayo amesema ingeweza kutekelezwa na sekta binafsi kuwa ni ujenzi wa reli ya kisasa ya kati, mradi wa umeme Rufiji, mradi wa bandari na uboreshaji shirika la ndege.
“Kama mpango huu utatekelezwa kama ulivyo, miradi hii inakwenda kuua uchumi wa nchi yetu. Miradi hii mikubwa inaweza kujiendesha kibiashara na ikajilipa yenyewe,” amesisitiza Nape.
Kwa mujibu wa Nape, miradi hiyo ni mikubwa na itagharimu fedha nyingi ambazo zitailazimisha Serikali kukopa fedha nyingi, hali ambayo itaathiri deni la taifa ambalo kwa sasa Dola bilioni 26.
“Serikali ikienda kukopa  na kwa sababu miradi hii inachukua muda mrefu maana yake tutaanza kulipa deni kabla ya miradi hiyo haijaanza kurudisha faida kwa taifa,” amesema katika mchango wake.
“Kuna madhara makubwa kwa deni la taifa. Ndio hapa ninapohoji uzalendo wa wachumi wetu katika kuishauri Serikali na Rais Magufuli katika kuchukua pesa za Serikali na kuwekeza katika miradi hii”.
“Kwa mujibu wa takwimu ripoti uliyotupa hapa, deni letu la taifa limefikia Dola 26 bilioni ambayo ni sawa na asilimia 32 ya ustahimilivu wa deni la taifa. Ukomo ni asilimia 56”.
“Sasa kama Dola bilioni 26 zimetupeleka kwenye asilimia 32 unahitaji Dola bilioni 45 kufikia ukomo wa asilimia 56 ambao ni mwisho wa kukopesheka. Tuchukue mifano ya miradi mitatu tu” amesema.
“Ujenzi wa reli ya Kati ambayo kwa tathmini yake unaweza kugharimu Dola bilioni 15. Stiegler’s  Gorge utagharimu Dola bilioni 5 na uboreshaji wa shirika la ndege karibia Dola bilioni 1”
“Kwa hiyo unazungumzia Dola bilioni 21. Ukijumlisha na deni la taifa la bilioni 26 unazungumzia Dola bilioni 47. Kwa vyovyote vile hii ime bust (imepasuka)”alisema Nape na kuongeza kusema;-
“Kama inakwenda ku bust maana yake tunakwenda kutokopesheka. Kwanini tunataka kung’ang’aniza kuchukua pesa ya Serikali”. Hebu tufikirie upya. Dk Mpango rudini mkafikiri upya”
Nape alisema kuanzia awamu ya pili chini ya Rais Alli Hassan Mwinyi hadi awamu ya nne, Serikali ilitengeneza mazingira mazuri ya kuishirikisha sekta binafsi katika miradi mbalimbali ya kiuchumi.
“Wakati wa awamu ya nne  Rais Magufuli alikuwa Waziri wa Ujenzi. Wakati wake waliruhusu wakandarasi kutoka sekta binafsi. Wakachukua mikopo benki wakaanzisha makampuni”
“Leo dhamana walizozitumia kukopa fedha  zinauzwa kwa sababu ya madeni wanayoidai Serikali lakini Serikali nayo imeanza mkondo wa miradi yake ya ujenzi kutekelezwa na Serikali yenyewe”
“Kwa hiyo hawa tuliowatengeneza kwa miaka yote tumewakosesha pesa. Huu mpango wako mzuri lakini rudini kwenye mawazo ya kutumia sekta binafsi. Tukienda hivi tunaenda kuua uchumi,”alisema.

No comments:

Post a Comment