Friday, November 10

Rodrigo Duterte: Rais wa Ufilipino akiri kwamba aliwahi kumuua mtu akiwa kijana

Duterte akielekea VietnamHaki miliki ya pichaEPA
Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte amekiri kwamba alimuua mtu kwa kumchoma kisu akiwa kijana.
"Nikiwa na miaka 16, nilimuua mtu," aliwaambia raia wa Ufilipino katika mji wa Da Nang nchini Vietnam ambako anahudhuria mkutano mkuu wa viongozi wa nchi za Asia na Pasifiki.
Amesema alimdunga kisu mtu huyo "kwa sababu ya kutazama tu".
Msemaji wake baadaye amesema tamko la kiongozi huyo lilikuwa "utani tu".
Bw Duterte amewahi kusema awali kwamba aliwaua washukiwa wa uhalifu alipokuwa meya wa mji wa Davao.
Kiongozi huyo wa Ufilipino anahudhuria mkutano huo wa Apec pamoja na viongozi wengine akiwemo Rais wa Marekani Donald Trump.
Bw Duterte anatarajiwa kushauriana moja kwa moja na Rais wa Marekani Donald Trump siku chache zijazo - mkutano wa kwanza kati ya wawili hao.
Rais huyo wa Ufilipino ameongoza kampeni yenye utata ya kukabiliana na wahalifu na walanguzi wa dawa za kulevya.
Wakosoaji wake wanasema kampeni hiyo imehusisha ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu.
Bw Duterte amewahamasisha watu kuua washukiwa wanaohusika na dawa za kulevya bila kuwafikisha kwa polisi na alisema anaweza kufurahia sana iwapo angeweza kuwaua waraibu milioni tatu wa mihadarati nchini humo.
Akihutubia raia wa Ufilipino mjini Da Nang, amesema alimuua mtu wakati wa ukali wake miaka yake ya ujana na kwamba kulikuwa na vita vingi pamoja na "kuingia na kutoka jela" mara kwa mara.
Lakini msemaji wake Harry Roque, ameambia AFP kwamba Duterte alikuwa anatania tu na kwamba kiongozi huyo mara nyingi hutumia "lugha iliyoongezwa chumbi" akihutubia Wafilipino nje ya nchi yake.
Obama na DuterteHaki miliki ya pichaEPA
Image captionRais Obama na Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte waangaliana mjini Laos
Bw Duterte aliwahi kusema kwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba alimuua mtu akiwa kijana.
Mwaka 2015, aliambia jarida la Esquire la Ufilipino kwamba wakati wa vita vikali ufukweni alipokuwa na miaka 17 "huenda nilimuua mtu kwa kumdunga kisu".
Haijabainika iwapo anazungumzia kisa hicho kimoja.
Amedai kwamba amewahi pia kuwarusha watu kutoka kwenye helikopta ikiwa angani.
Tangu achukue hatamu, polisi wanasema wamewaua watu karibu 4,000 katika operesheni ya kukabiliana na walanguzi wa mihadarati.
Watu wengine zaidi ya 2,000 wameuawa kwa makosa yanayohusiana na dawa za kulevya.
Trump atazuru Ufilipino akikaribu kumalizia ziara yake barani Asia.
Bw Duterte alizua utata alipomwelezea mtangulzii wa Trump, Barack Obama kama "mwana wa kahaba".
Bw Obama alifuta mkutano uliokuwa umepangwa kati ya wawili hao.

No comments:

Post a Comment