Friday, November 10

Shule ya Kihinga yafungwa kwa muda


Ngara .Uongozi wa  Shule ya Msingi  Kihinga umaamua kuifunga kwa muda shule hiyo kwa lengo la kuwajenga kisaikolojia wanafunzi wake baada ya wenzao kupoteza maisha kutokana na mlipuko wa bomu.
Akizungumza  Mwananchi leo Novemba 10 ,Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Aidan Makobero amesema   shule hiyo imefungwa kimasomo hadi Jumatatu ili wanafunzi waweze kupata malezi ya  kisaikolojia
Aidha amesema kwa shule jirani  ya Nyarukubala iliyo karibu na mpakani na  Burundi mahudhurio yamepungua kutoka wanafunzi 700  na kufikia 100  leo  Novemba 10
“Hata shule nyingine ya Nyarulama nayo wanafunzi wake wamepungua  baada ya tukio la shuleni kwangu na kusalia majumbani wakiogopa kwenda shule wakidai nao wanaweza kukumbwa na tukio  kama la shule jirani’’ amesema  Makobero
Pia majeruhi 33 kati ya 42 waliojeruhiwa kwa bomu wameruhusiwa na kurejea makwao baada ya afya zao kuimarika
Mganga wa hospitali ya misheni ya Rulenge Dk Mariagoleth Frederick amesema majeruhi hao  ni wanafunzi wa shule ya msingi Kihinga wilayani humo wameruhusiwa  na kubaki majeruhi 11
Amesema majeruhi waliosalia watano baada ya kufanyiwa uchunguzi bado kwenye sehemu za mifupa kunaonekana kuwepo vipande vya bomu na jitihada zinafanyika kuondoa vipande hivyo
Amesema wengine sita wanaendelea kuhudumiwa na mpaka sasa zimepatikana uniti 67 za damu kutoka kwa  wasamaria wema wakiwemo wanafunzi wa sekondari ya Mbuba Rulenge na vijana waendesha pikipiki
Aidha amesema shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR tawi la Ngara limetoa blanketi  60 kwa  zahanati jirani, MSD wilaya ya Muleba na ofisi ya mganga mkuu wa mkoa vilitolewa vifaa tiba na dawa.
" Changamoto kubwa ni jinsi ya kumudu watoto hao kwa kuwapatia chakula hivyo ombi ni wasamaria wema kusaidia chakula maana wazazi wao hawana uwezo kiuchumi " Amesema
Pia amesema mwalimu wa shule hiyo aliyejeruhiwa Policaripo Clemens naye ameruhusiwa na kwamba jopo la madaktari linashughulikia majeruhi hao watano ambao hali ikishindikana watapewa rufaa hadi Bugando.
Mwenyekiti  wa kijiji cha Kihinga Hasan Mohamed amesema  idara ya mali asili na kamati za ulinzi na usalama zingeondoa vivuko  mto Ruvubu unaounganisha Tanzania na Burundi kuzuia watu kuvuka  kutoka na kuingia  mataifa hayo

No comments:

Post a Comment