Friday, November 10

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda awataka wafanyakazi waache mazoea


Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Profesa Elisante Ole Gabriel amekutana na wakuu wa taasisi zilizo chini ya wizara hiyo leo Novemba  9 na kuwataka kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili kuleta matokeo yanayotarajiwa.
Profesa Gabriel amesema wizara hiyo imepewa majukumu makubwa ya kusimamia utekelezaji wa azma ya serikali ya kujenga uchumi wa viwanda, kwa hiyo ili kufikia malengo hayo lazima utendaji wa watumishi wa umma ubadilike.
Amesema hatavumilia uzembe wa aina yoyote ambao utakwamisha serikali kufikia malengo yanayotarajiwa. Amewataka kuwasimamia watendaji katika taasisi zao na wajipange kutoa huduma kwa saa 24.
Kiongozi huyo amewataka wakuu hao wa taasisi kuandaa mpango kazi ifikapo Novemba 30 ambao utawawezesha kufanya kazi kwa saa 24. Amesema waangalie pia kuwa na simu za bure kwa ajili ya kusikiliza wateja au wawekezaji.
"Tunataka discipline (nidhamu) kwenye taasisi mnazozisimamia. Utamaduni wa kufanya kazi kwa mazoea sasa ufikie mwisho, tuanze kufanya kwa saa 24 kwa wiki," amesema katibu mkuu huyo ambaye Oktoba 26 alihamishwa kutoka wizara ya habari.
"Hatuwezi kushindana kwenye soko huria la Afrika Mashariki kama tutaendelea kufanya kazi kwa mazoea. Nitafanya kazi chini ya falsafa ya 'fast' kwa maana ya kufanya kazi kwa haraka, ukweli na kimkakati," amesema.
Amesisitiza kwamba mazingira ya Tanzania ya kisiasa, kijamii, kiuchumi na kiteknolojia yako vizuri, hivyo hakuna sababu ya kushindwa kufikia malengo yao kwa wakati.
Baadhi ya taasisi zilizo chini ya wizara hiyo na zilizowakilishwa katika mkutano huo ni pamoja na TBS, TIC, Brela, TanTrade, FTC, TIRDO, Cosota na chuo cha CBE.

No comments:

Post a Comment