Naibu ofisa mtendaji mkuu wa Sagcot, Jennifer Baarn alisema iwapo Rais atauangalia ushoroba huo utasaidia kufikia Tanzania ya viwanda.
Jennifer ambaye anamaliza muda wake katika nafasi hiyo alisema kuwa kitu pekee atakachokikumbuka kwa miaka sita aliyokaa Tanzania ni kufanya kazi na watu wanaopenda kujifunza na kuifikisha nchi juu kiuchumi.
“Namuomba Rais Magufuli kusaidia shughuli za Sagcot katika ushoroba wa Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania na hasa katika masuala ya miundombinu na shughuli za kongani. Vilevile asaidie watendaji wa Serikali ambao tunashirikiana nao katika kuinua kilimo nchini,” alisema Baarn.
“Nitakumbuka vitu viwili, kwanza kufanya kazi, tena kufanya kazi na watu wanaosoma kwa bidii ili kusaidia maendeleo ya nchi yao katika nyanja mbalimbali. Kingine nitakachokikumbuka ni Bagamoyo, naupenda mji ule mkongwe ambao ulikuwa kama nyumbani.”
Mbali ya mafanikio aliyoyapata kwa miaka sita aliyokuwa kwenye kituo hicho kinachofanya kazi kwa ubia kati ya sekta binafsi na ile ya umma, Baarn alisema zipo changamoto kadhaa za kiutendaji ambazo zikipatiwa ufumbuzi Tanzania itakuwa sehemu salama kwa chakula.
Alisema, hakuna uwiano katika utendaji wa kazi hasa zinazowagusa wakulima wadogo na mambo mengi wanayotwishwa kwa wakati mmoja hadi wanachanganyikiwa na kushindwa kufuata lipi kwa wakati gani.
Mkazi wa Tukuyu mkoani Mbeya, Mwasele Kalipingu alisema uzalishaji katika sekta ya kilimo unakwazwa na pembejeo ambazo huwa hawazipokei kwa wakati na wakati mwingine hazitoshelezi.
“Ukanda huu wa Nyanda za Juu Kusini pia una maeneo mengi ambayo kupitika nyakati za mvua hususan vijijini ni shinda,” alisema.
No comments:
Post a Comment