Monday, November 27

Ubomoaji jengo la Tanesco waanza


Uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) umesema umeanza utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli la kubomoa jengo lake lililo ndani ya hifadhi ya barabara eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam.
Kazi hiyo iliyoanza leo Jumatatu Novemba 27,2017 ni utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli aliyeagiza majengo ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji na ghorofa la Tanesco kuwekwa alama ya X kwa ajili ya kubomolewa.
Novemba 15,2017 akitokea Chato alipokwenda kwa mapumziko baada ya ziara ya Uganda, Rais Magufuli aliagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuweka alama ya X katika majengo hayo sehemu zilizo katika hifadhi ya barabara.
Taarifa ya Tanesco kwa umma imesema kuanzia leo Jumatatu Novemba 27,2017 wameanza kubomoa ukuta wa mbele ya jengo.
Tanesco imesema baadhi ya watumishi wa shirika hilo wameanza kuhamishiwa katika ofisi nyingine za shirika zilizopo jijini Dar es Salaam ili kupisha shughuli za ubomoaji kufanyika kwa usalama.
Uongozi wa shirika hilo na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) unaendelea kufanya utaratibu utakaowezesha ubomoaji wa jengo hilo la ghorofa kufanyika bila kuathiri huduma kwa wateja wa Tanesco.
“Katika kipindi hiki cha utekelezaji wa agizo la Rais. Tunapenda kuwahakikishia wateja  na Watanzania kwa jumla kuwa, huduma za umeme zitaendelea kupatikana kama kawaida ikiwemo huduma ya ununuzi wa Luku,” imesema taarifa hiyo.
Uongozi wa shirika hilo umesema utaendelea kutoa taarifa kwa kadri kazi hiyo itakavyokuwa ikiendelea.

No comments:

Post a Comment