Monday, November 27

Dart inalenga kuwa na mabasi 305


Dar es Salaam. Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), unatarajia kuongeza mabasi katika mfumo wake kutoka 140 yaliyopo sasa hadi 305 pindi awamu ya kwanza ya mfumo huo itakapokamilika Juni 2018.
Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Novemba 27,2017 kwa vyombo vya habari imemkariri Mtendaji Mkuu wa Dart, Ronald Lwakatare akitoa kauli hiyo baada ya kupokea wageni sita kutoka Serikali ya Rwanda waliokuja nchini kwa ziara ya siku tano kujifunza namna wakala huo unavyotoa huduma.
Mhandisi Lwakatare amesema kuongeza mabasi kutaongeza idadi ya abiria kutoka 200,000 kwa siku hadi kati ya 400,000 na 500,000 kwa siku.
“Mbali na hilo pia tutaongeza njia za mlisho kutoka mbili zilizopo sasa hadi tisa zitakazokuwa zikienda Masaki, Sinza, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam  na maeneo mengine ambayo yapo jirani ili kupanua huduma ya usafiri katika maeneo yaliyomo ndani ya mfumo wa mabasi yaendayo haraka katika awamu ya kwanza ya mradi,” amesema Mhandisi Lwakatare.
Pia, amezungumzia athari iliyotokana na mvua iliyonyesha Oktoba 26, akisema mfumo wa mabasi uliathiriwa kwa kuwa mabasi 20 yaliharibika zaidi lakini yameshatengezwa na kuanza kutoa huduma.
Amesema Dart imejipanga kuhakikisha mitaro yote inayozunguka karakana ya Jangwani inasafishwa ili kuepuka eneo hilo kukumbwa tena na mafuriko.
Kuhusu wageni hao, Mhandisi Lwakatare amesema wamekuja kujifunza kuhusu mradi huo na hatua waliyoifikia Dart ikizingatiwa Jiji la Kigali lina mpango wa kuwa na mfumo kama huo.
Kiongozi wa ujumbe huo kutoka Mamlaka  ya Halmashauri ya Jiji la Kigali, Rwagatore Etienne amesema wameamua kuchagua kutembelea wakala huo kwa sababu ndiyo mradi uliofanikiwa barani Afrika na upo karibu na nchi ya Rwanda.
Katika msafara, Etienne ameambatana na  wataalamu washauri ambao ndio waliopewa kazi ya usanifu wa Jiji la Kigali ili liweze kuwa na mfumo wa mabasi yaendayo haraka.

No comments:

Post a Comment