Thursday, November 16

Mjadala wenye thamani bungeni wafunikwa na sinema ya Dk Shika


Hoja nzuri na zenye thamani kubwa zilichomoza bungeni wakati wa mjadala wa Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2017/18. Baadhi ya wabunge walisimama na kulinda thamani na heshima ya Bunge kama yalivyo matakwa ya Katiba.
Mambo muhimu yaliyochanua ni kupaa kwa Deni la Taifa, Mpango wa Maendeleo kutoakisi hali halisi ya nchi, wakulima kusahaulika, Serikali kujielekeza kwenye kukusanya kodi na kubana badala ya kutanua uzalishaji.
Jambo jingine ambalo lilijadiliwa ni madai ya upindishwaji wa takwimu za Serikali, kukiwa na mkanganyiko kutoka mwaka mmoja hadi mwingine, vilevile tarakimu kupishana.
Ni hoja ambazo zinapaswa kumpa sura mbili kila Mtanzania. Ya kwanza ni ndita; kwamba Serikali haitumii sayansi katika utawala ndiyo maana Wizara ya Fedha imewasilisha bungeni Mpango wenye kasoro nyingi. Ya pili ni tabasamu; kwamba wabunge wanatimiza wajibu wao wa kuisimamia Serikali.
Wakati wabunge wakipaza sauti kueleza athari na maumivu ya kiuchumi kwa nchi kupitia kasoro ndani ya Mpango mpya na kutotekelezwa ipasavyo kwa mipango iliyopita, nchi kwa sehemu kubwa ya watumia mitandao ya kijamii, ilijielekeza kujadili tukio la mnadani.
Alhamisi ya Novemba 9, kampuni ya udalali ya Yono ilifanya mnada wa nyumba tatu za mfanyabiashara Said Lugumi anayedaiwa malimbikizo ya kodi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Nyumba hizo, mbili zipo Mbweni, Kinondoni na Upanga, Dar es Salaam.
Katika mnada huo, alijitokeza mtu aliyejitambulisha kwa majina ya Dk Louis Shika ambaye alishinda mnada wa kununua nyumba zote tatu kwa Sh3.2 bilioni. Moja Sh900 milioni, nyingine Sh1.1 bilioni na ya tatu Sh1.2 bilioni. Baada ya kushinda akapepewa na kushangiliwa.
Taarifa za ushindi wa Dk Shika zilipovuja tu, picha yake ilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, huku sifa kuu akipambwa kuwa si mtu mwenye wajihi wa kuogopesha au wa kitajiri, bali mwonekano wake ni wa kawaida tu, lakini amethibitisha ni bilionea kwa kununua majumba ya Lugumi.
Sheria ya minada nchini inaelekeza kwamba ukishinda kununua mali husika, unapaswa kulipa papohapo asilimia 25 ya bei uliyoshinda kununua, asilimia 75 inayosalia hulipwa ndani ya siku 14. Hivyo, kwa nyumba tatu ambazo Dk Shika alishinda kuzinunua kwa Sh3.2 bilioni, alipaswa kulipa mara moja Sh800 milioni ambazo ndiyo asilimia 25.
Zikafuatia taarifa kuwa Dk Shika hakuwa na Sh800 milioni za kulipa siku hiyo. Ikabainishwa kuwa mtu huyo ama alijituma au alitumwa kukwamisha mnada. Taarifa za polisi zilikwenda mbali zaidi na kueleza kuwa Dk Shika ni tapeli. Hizo ni tuhuma na sheria bila shaka itachukia mkondo wake.
Hoja ni kuona kuwa sinema ya mnadani, iliyochezwa na Dk Shika, ilipata mapokeo makubwa na kujadiliwa na watu wengi kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kwa jumla, kuliko kilichojiri bungeni kulikokuwa na mjadala wenye hadhi kubwa kwa Taifa.
Kilichokuwapo bungeni
Siku Dk Shika alipocheza sinema yake mnadani, ndiyo ambayo Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM), Peter Serukamba alibainisha mkanganyiko wa takwimu za Deni la Taifa. Mpango wa mwaka 2016-2017, ulieleza kuwa mpaka Oktoba 2015, deni lilikuwa dola 19 bilioni (Sh42.8 trilioni), ikiwa limeongezeka kutoka dola 18 bilioni (Sh40.5 trilioni) mwaka 2014.
Serukamba alibainisha kuwa taarifa ya Mpango uliopita, kulikuwa na maelezo kuwa Deni la Taifa lilifikia dola 18 bilioni (Sh40.5 trilioni), ikiwa ni ongezeko la asilimia 9.76 kutoka Oktoba 2015 ambako deni lilikuwa dola 16 bilioni (Sh.36 trilioni). Hapo kwa hakika kuna mkanganyiko wa haja.
Serukamba alibainisha pia kuwa Mpango mpya unasema Deni la Taifa limefikia dola 26 bilioni (Sh58.6 trilioni) hadi Juni mwaka huu, kutoka dola 22 bilioni (Sh49.6 trilioni) Juni 2016. Taarifa iliyopita inasema Oktoba 2016 deni lilikuwa Sh40.5 trilioni, mpya inaeleza Juni 2016 deni lilisoma Sh49.6 trilioni.
Mshangao ni kwamba taarifa zote zinaandikwa na Wizara ya Fedha. Hapo ndipo shaka inakuwepo kuhusu utendaji wa watu ambao wamekabidhiwa majukumu ya kiutendaji kuhusu nchi. Je, ni umakini mdogo? Kufanya bora liende au makusudi kupindisha takwimu?
Mchango wa Serukamba uligusa pia namna Mpango wa Maendeleo ulivyoiacha sekta binafsi na kilimo. Alieleza jinsi ambavyo Serikali inanadi nchi ya Viwanda wakati kwenye Mpango hakuna tamko la kuongeza tija kwenye kilimo, zaidi inazungumzwa kubana na kukusanya kodi bila kuweka mipango ya uzalishaji.
Alitoa mfano kwamba Bangladesh kiwanda kimoja kinatumia pamba robota 5,000,000, wakati Tanzania inahubiriwa kubadilika kuwa nchi ya viwanda kwa kutegemea mavuno ya pamba robota 240,000. Ni hapo Serukamba aliuliza: “Tunamdanganya nani hapa?”
Bashe na Nape
Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye alizungumzia kasoro ya Serikali kutoishirikisha sekta binafsi katika miradi inayoweza kujiendesha kibiashara, badala ya kuendelea kukopa, kitu ambacho alionya kwamba kitakuja kusababisha athari kubwa kwa nchi.
Jambo la kwanza Nape alisema kuwa Serikali inakopa fedha nyingi kwa ajili ya miradi mikubwa ambayo ukamilikaji wake unachukua muda mrefu, wakati mikopo husika marejesho yake yanafanyika ndani ya muda mfupi. Kutokana na hali hiyo, alitahadharisha kwamba marejesho yataathiri miradi mingine.
Nape alisema kwa vile miradi itachelewa kukamilika, wakati wa marejesho ya mikopo, itabidi kuchukua fedha kwenye miradi ya huduma kama elimu, afya na kadhalika ili kuwalipa wadeni wa nchi. Katika hili Nape alisema anatilia shaka uzalendo wa wachumi ambao wanamshauri Rais.
Upande wa pili, Nape alionya kuwa nchi inapiga hatua kwenda kuwa isiyokopesheka ikiwa itakopa kwa ajili ya miradi miwili tu; wa kwanza ni ujenzi wa reli ya kisasa na wa ufuaji umeme wa Stiegler’s Gorge megawati 2,100.
Nape alisema taarifa za Mpango mpya zinaeleza Deni la Taifa limefikia dola 26 bilioni (Sh58.6 bilioni) sawa na asilimia 32 ya uhimilivu wa deni. Kwamba ili Tanzania ifikie kikomo cha kukopeshwa, deni lake linapaswa kufikia dola 45 bilioni (Sh101.4 trilioni).
Kutokana na hoja hiyo ya Nape, anasema endapo Serikali itaongeza mkopo kwa miradi miwili tu ya standard gauge na Stiegler’s Gorge, itafika kwenye kiwango chake cha mwisho cha kukopa.
Hoja ya Bashe iligusa kuporomoka kwa wastani wa ukuaji wa Pato la Ndani la Taifa (GDP) na Benki Kuu kutoripoti kiwango cha uingizaji na usafirishwaji wa bidhaa nje ya nchi, tangu Juni mwaka huu ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya nchi.
Bashe pia alizungumzia Mpango wa Maendeleo kukosa mkazo kwenye sekta ya kilimo kuwa Serikali inadhibiti mfumuko wa bei kwa kumkandamiza mkulima, vilevile alikosoa mipango ya viwanda kwamba haiendani na hali halisi.
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alitaka wabunge wa CCM kuwa imara zaidi kwa kile alichoeleza kwamba nchi inakwenda vibaya na wao ndiyo wenye dhamana kubwa kama chama tawala.
Aliwapongeza Serukamba na Bashe kwa kuamua kuwa wakweli na kuzungumza hali halisi kuhusu mwenendo wa uchumi kwa nchi.
Ndugai aliwasema wabunge wa CCM kuwa hawatakiwi kuunga mkono tu kwa sababu CCM ndiyo kabisa haitaki mipango mibaya. Kimsingi Ndugai alichokimaanisha ni Bunge analoliongoza kuwa la hoja zenye mantiki kwa faida ya nchi na siyo kuwachekea mawaziri ikiwa wanapeleka bungeni hoja zenye kasoro nyingi.
Alichokizungumza Ndugai kuwaamsha wabunge kujadili Mpango wa Maendeleo kwa uwazi na bila woga, alikopita Serukamba na hoja zilizojengwa na Nape, Bashe na Mbowe, kwa pamoja ndiyo tafsiri ya Bunge la kisasa. Bunge lenye kuyatangulia maisha ya watu.
Kimsingi hoja za vikao vya Bunge kuanzia Alhamisi iliyopita mpaka Ijumaa, ndizo ambazo zilipaswa kung’ara na kutembea zaidi kwenye mitandao ya kijamii na kwenye vyombo vya habari kwa jumla. Kinyume chake Dk Shika na sinema yake ya mnadani akafunika mjadala bora mno kwa maslahi ya Watanzania.   

No comments:

Post a Comment