Thursday, November 16

Ajali ya boti yahofiwa kuua wawili


Kagera. Watu wawili wanasadikika kufa maji baada ya boti ya mizigo ya Mv Julias kuzama majini wakitoka kisiwa cha Goziba katika ziwa Viktoria mkoani Kagera kuelekea jijini Mwanza.
Diwani wa Kata ya Goziba, Masaba Nkunami amesema boti hiyo imezama usiku wa kuamkia leo Alhamisi muda mfupi baada ya kuanza safari zake kutoka kisiwani hapo.
Licha ya kutotaja idadi kamili ya watu waliokuwamo kwenye boti hiyo ya mizigo, Nkunami amesema kwa sasa wanaendelea na jitihada za kuwatafuta watu wawili wanaosadikika kuzama ziwani.
Amesema boti hiyo iliundwa kwa vyuma mfano wa meli ambayo hufanya shughuli za kusafirisha mizigo kati ya kisiwa cha Goziba na Mwanza.
“Jitihada za kutafuta watu hao zinaendelea hadi sasa watu wapo majini wakiwatafuta, hivyo taarifa zaidi zitatolewa baadaye,” amesema Nkunami.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi amekiri kuzama kwa boti hiyo lakini akasema “mpaka sasa hakuna taarifa za vifo.”

No comments:

Post a Comment