Thursday, November 16

Wabunge wapinga majukumu ya ‘Nasaco’ mpya

By Sharon Sauwa, Mwananchi ssauwa@mwananchi.co.tz
Dodoma. Wabunge wamepinga Shirika la Taifa la Wakala wa Meli (Nasac) kupewa majukumu ya kufanya biashara na udhibiti kwa sababu yanasababisha mgongano wa maslahi kwa yenyewe kuwa mdhibiti na wakati huo huo kufanya kazi ya uwakala wa meli.
Kuundwa kwa shirika hilo jipya kunakuja baada Serikali kubinafsisha Kampuni ya Wakala wa Meli (Nasaco) mwaka1998 ambayo ilidumu kwa miaka 25.
Kauli hiyo imekuja mara baada ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliani Profesa Makame Mbarawa kuwasilisha bungeni Muswada wa Sheria ya Wakala wa Meli wa Taifa ya Mwaka 2017 ambayo inaunda shirika hilo na kuainisha majukumu yake.
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Miundombinu leo Alhamisi, makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, Moshi Kakoso amesema kamati imebaini kuwa Nasac inayopendekezwa itakuwa na jukumu la udhibiti na kufanya kazi za uwakala.
“Kamati inashauri kuwa ni vyema Serikali ikatenganisha masuala ya udhibiti na ufanyaji wa biashara ili kuweza kuondoa mgongano wa kimaslahi kwa mdhibiti kufanya kazi uwakala,” amesema.
Kakoso amesema pia sheria iliyokuwepo awali ilikuwa inaruhusu wakala wa meli kuwa pia wakala wa mizigo.
Hata hivyo, amesema sheria inayopendekezwa kifungu cha 38(2) (a) kinachohusu utoaji leseni kwa mawakala wa meli hakiruhusu mwenye meli kupewa leseni ya uondoshaji wa shehena.
“Kamati inaona kuwa hakuna sababu za msingi za kuzuia hii kwani ni ngumu sana katika dunia ya sasa kuepuka muungiliano huo. Jambo la msingi ni kuwa ni kuwa na udhibiti na ufuatiliaji wa karibu ili kuepuka ubadhilifu ambapo awali ulikuwa unajitokeza,” amesema.
Vifungu hivyo pia vilipingwa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ambapo wamesema muswada huo unalipa shirika hilo mamlaka makubwa ya kuweza kuiua sekta ya usafirishaji wa majini kwa kuwa mdhibiti lakini wakati huo huo mtoa huduma za uwakala.
Msemaji wa kambi hiyo, Suzan Lyimo amesema kuna hoja ambazo zinaletwa kwa nguvu zote ili kupitisha muswada hatari ikiwa sababu za udanganyifu wa shehena iliyomo katika meli kuwa sio inayotakiwa kulipiwa ushuru.

No comments:

Post a Comment