Thursday, November 16

Mawakili wa utetezi kesi ya bilionea Msuya waingiwa hofu bastola ya askari


Moshi. Mahakama Kuu imesimama kwa muda kesi ya mauaji ya bilionea Erasto Msuya baada ya shahidi wa 16, PF 1878 Willium Mziu, ambaye ni  mkaguzi wa polisi upelelezi makao makuu kuingia na bastola mahakamani hali ambayo ilileta hofu kwa mawakili  upande wa utetezi.
Hali hiyo iliyotokea leo Alhamisi imesababisha wakili upande wa utetezi, Hudson Ndusyepo kuiambia mahakama hiyo kuwa hawawezi kuendelea kusikiliza kesi hiyo kutokana na shahidi huyo kuonekana na silaha na kumwambia Jaji Salma Maghimbi kuwa hawapo salama.
Kwa upande wake wakili upande wa mashtaka, Abdallah Chavula ameiambia mahakama hiyo kuwa shahidi huyo anaruhusiwa kuingia na silaha mahakamani kutokana na kwamba yeye ni ofisa wa polisi.
Hata hivyo, muda kidogo Jaji Salma Maghimbi aliahirisha kusikilizwa kwa kesi hiyo muda wa nusu saa moja.
Kesi hiyo ya mauaji ya kukusudia inasikilizwa na Jaji Maghimbi ikiwa na washtakiwa saba ambao ni Sharifu Mohamed, Shaibu Jumanne, Musa Mangu, Jalila Zuberi, Karimu Kihundwa, Sadik Mohamed na Ally Musa.

No comments:

Post a Comment