Jimbo la Singida Kaskazini liliachwa wazi baada ya Mbunge wake, Lazaro Nyalandu kutangaza kujiuzulu wakati Longido likiachwa wazi baada ya Mahakama Kuu kutengua matokeo ya uchaguzi wa mbunge wake, Onesmo Ole Nangole.
Taarifa ya Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage imesema mbali na majimbo hayo, zipo kata nyingine tano zilizo wazi zitakazopaswa kufanya uchaguzi huo mdogo.
Kaijage amesema tayari tume hiyo imepokea taarifa kutoka kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai juu ya kuwepo kwa nafasi wazi ya Ubunge katika Jimbo la Singida Kaskazini baada ya Nyalandu kuvuliwa uanachama wa CCM na hivyo kupoteza sifa ya kuwa Mbunge.
Amesema kwa kuzingatia masharti ya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, tume hiyo itatoa ratiba ya uchaguzi wa kujaza nafasi wazi za Majimbo hayo na kata hizo baadaye.
“Aidha, kwa mujibu kifungu cha 113(1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, Tume imepokea Hati ya Mahakama Kuu ya Tanzania ikithibitisha uamuzi wa Mahakama hiyo juu ya kutengua matokeo ya Uchaguzi wa Mbunge wa Jimbo la Longido ambalo, Onesmo Ole Nangole alikuwa ni Mbunge,” ameeleza Jaji Kaijage kwenye taarifa yake.
Katika hatua nyingine, tume hiyo imesema Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa kwa kutumia mamlaka aliyopewa chini ya kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, ameitaarifu uwepo wa nafasi wazi za madiwani katika Kata tano zilizopo katika Halmashauri mbalimbali nchini.
Taarifa hiyo imezitaja kata zilizowazi kwamba ni Keza mkoani Kagera, Kimandol (Arusha), Kurui mkoani Pwani, Bukumbi ,mkoani (Tabora) na Kwagunda ,(Tanga).
No comments:
Post a Comment