Sunday, March 11

Supermarket zatii katazo la nyama kutoka Afrika Kusini


Idadi kubwa ya maduka makubwa ya bidhaa (supermarkets) yametii agizo la Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania, (TFDA) la kuzuia uingizaji nyama kutokana Afrika Kusini.
Hatua hiyo imekuja baada ya soseji, zinazotengenezwa huko aina ya Polony kubainika kuwa na ugonjwa wa listeriosis uliosababisha vifo vya watu 180 nchini humo.
Soseji hizo, zinatengenezwa na kiwanda cha Tiger Brands Unit Enterprises na cha RCL Foods vya Afrika Kusini.
Katika taarifa yake Machi 7, TFDA ilisema usitishaji utaendelea hadi hapo itakapothibitishwa kuwa bidhaa hizo ni salama.
Baada ya taarifa hiyo, mwandishi wetu alitembelea maduka makubwa ya vyakula ya Shrijees lililopo Masaki, Mkuki House (Keko Darajani), Imalaseko (Posta) na Food Lovers la Oysterbay na kote huko bidhaa za nyama kutoka Afrika Kusini hazikuwapo.
Pia alibaini kuwa nyama za kusaga na soseji kutoka nje ya nchi zipo kwa kiasi kidogo na nyingi zinatoka Kenya.
Msemaji wa TFDA, Gaudencia Simwanza alisema bado wanaendelea na uchunguzi kubaini kama bado kuna maduka yanayouza soseji na nyama za kusaga kutoka nchini humo.
Hata hivyo alisema, “Sisi tulitaja kampuni yenye vyakula vyenye hilo tatizo, hivyo wananchi walizingatie hilo pia. Tunaendelea na kazi ya ukaguzi ndani na mipakani kuona kama bidhaa hizo bado zinaingizwa nchini, tutakachokibaini tutawafahamisha.”
Mmoja wa wateja aliyekutwa akinunua bidhaa katika duka la Food Lovers, Mwahija Haji alisema tangazo la uwepo wa nyama kutoka Afrika Kusini zenye bakteria limewaamsha na kuwa makini wanapokuwa madukani.
“Nasoma kabla sijanunua na kujiridhisha, hata ikiwa ya Afrika Kusini naangalia jina la kampuni ili nisinunue kutoka katika kampuni iliyotajwa” alisema Mwahija.
Alisema kuwa ili kuepuka usumbufu huo, ananunua zinazozalishwa hapa nchini ingawa alidai kuwa baadhi hazina ubora.
Mlipuko wa listeriosis ulianza Desemba mwaka jana na mpaka sasa umesababisha vifo vya watu 180 huko Afrika Kusini.
Akiuchambua ugonjwa wa listeriosis, Dk George Kanani wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza alisema ni aina ya bakteria ambao hupatikana kwenye maji, ubongo na kinyesi.
Alisema binadamu huambukizwa pale wanapotumia vyakula au maji yenye bakteria hao.
“Sababu kuu zinazosababisha listeriasis ni nyama na maziwa mabichi,” alisema.
Dk Kanani alisema bakteria hao ni hatari na huweza kusababisha kifo pale wanaposhambulia mfumo wa fahamu na wa damu.

No comments:

Post a Comment