Sunday, March 11

Fanya hivi kujenga mahusiano bora na mfanyakazi wa nyumbani


Tunakubaliana kuwa wafanyakazi wa nyumbani ni mhimili mkubwa majumbani hasa kwa wengi wetu tulioajiriwa kwenye sekta ama za umma au binafsi – hata wale waliojiajiri. Ipo wazi kwamba tunatambua umuhimu wa wasaidizi hawa katika kutekeleza majukumu ya nyumbani pindi tunapoondoka kwenda kazini na hata tuwapo majumbani. Tatizo lipo kwenye mahusiano yetu na hawa wasaidizi wetu majumbani.
Uzoefu unaonyesha kuwa wafanyakazi wa nyumbani hawadumu katika ajira zao. Leo yupo, kesho hataki tena kazi, anataka kurudi kwao. Wengine hawatulii ndani ya nyumba kutwa kuzurura mtaa hadi mtaa huku kazi na huduma kwa watoto zikilegalega. Vitendo vya namna hii huwaweka waajiri wao katika hali ya taharuki pasi na hakika ya huduma zinazotolewa na wafanyakazi wa namna hii.
Tambua kama waajiri ni muhimu sana kutambua kuwa wafanyakazi wa nyumbani hutofautiana, kila mtu huvaa uhusika tofauti na sifa ambazo huathiri utendaji wao wa kazi. Kujenga mahusiano mazuri na mfanyakazi wa nyumbani kuna faida kubwa kwani kufanya hivyo ni kumuongezea ufanisi katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku.
Tafiti zinaonyesha kwamba kukosekana kwa mahusiano mazuri kati mwajiri na mfanyakazi ni chanzo cha wasiwasi na migogoro inayojitokeza makazini mwetu. Vivyo hivyo hata majumbani mwetu sisi kama waajiri tunahitaji kuhuisha mahusiano ili mazingira ya kazi yawe rafiki.
Mlipe mshahara mzuri. Mshahara mzuri ni kichocheo katika kufanya kazi kwa bidii na weledi. Hatuna budi kutambua kwamba wafanyakazi wa nyumbani hutegemea mishahara tunayowalipa kwa ajiri ya kujikimu. Aidha hutumia pesa hizo kwa kusaidia familia zao kwani wengi wao hutokea kwenye familia duni na zisizojiweza. Tatizo linakuja pale tunapowapangia kazi lukuki huku tukiwalipa mishahara isiyolingana na majukumu wanayoyatekeleza. hapa ndipo mgongano unapoibukia.
Mawasiliano mazuri. Lugha ya staha na busara itumike wakati wa kuzungumza na mfanyakazi wako wa nyumbani na hasa wakati wa kutoa maagizo. Ugomvi na kumkaripia siyo njia bora za kutumia wakati wa kuwasiliana naye kwani kutaleta uhasama kadiri siku zinavyozidi kwenda. Hakikisha unampa maelekezo sahihi ambayo hayataweza kumchanganya na endapo utakugundua kuwa anafanya kosa kwenye jambo fulani, basi msahihishe katika njia ambazo hazitaonyesha kumdharau.
Usimbague. Onyesha unauthamini mchango wake kwa kumfanya sehemu ya familia hasa unapopata wasaa wa kununua vijizawadi nyumbani usimsahau walau mara moja moja.
Upo ushahidi wa kutosha wazazi tunawanunulia watoto wetu nguo nzuri ilihali mfanyakazi wa nyumbani unamletea nguo kuukuu. Kwanini umbague? Mfanye ajue kuwa unamthamini kwani itasaidia katika kujenga uhusiano bora baina yake na hata kwa watoto wako pia.
Mheshimu. Hakikisha mfanyakazi wa nyumbani haonewi pasi sababu. Watoto, ndugu na jamaa zako wampe heshima inayostahili. Asitukanwe na mtoto wako na ukakaa kimya. Asisumbuliwe na wageni wako na ukaa kimya. Huyu anakaa na watoto wako ukiwa haupo hivyo ni vyema umpe heshima. Atakulipa heshima. Mlipe dharau na madhara yake yataonekana!
Haya ni baadhi tu ya mambo unayoweza kufanya kujenga mahusiano na mfanyakazi wako wa nyumbani. Hatusemi ukimpa haya basi uhakika wa kuhusiana naye vyema upo asilimia 100. Bado unaweza ukampa kila atakacho pamoja na heshima na ukorofi atakuonyesha. Hili lisikuulie moyo wa utu wema.

No comments:

Post a Comment