Katika tamko la baraza hilo, limelaani tukio la Machi 7,2018 katika Hospitali ya Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara ambalo muuguzi Amina Nicodemus aliwekwa ndani kwa amri ya mkuu wa wilaya akituhumiwa kuuza nguo za watoto akiwa kazini.
Tukio lingine ni la Machi 8,2018 lililotokea katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga ambako muuguzi Hilda Ebunka alipigwa na diwani akiwa kazini.
Katika tamko lililotolewa leo Jumapili Machi 11,2018 na Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, Lena Mfalila limeeleza vitendo hivyo ni udhalilishaji na ni kinyume cha miongozo ya kisheria inayosimamia ushughulikiaji wa tuhuma za uvunjifu wa nidhamu na sheria wakati wa kazi.
"Kumpiga mtumishi wakati akiwa kazini ni udhalilishaji na ni kinyume cha sheria. Nidhamu ya wauguzi na wakunga inasimamiwa na sheria inayotoa mamlaka ya kuchukua hatua za kinidhamu kwa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania," amesema Mfalila.
Viongozi wa kitaifa, wakiwamo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tamisemi, Selemani Jafo; na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kwa nyakati tofauti wamekemea matukio hayo.
"Kwa tamko hili baraza linalaani vitendo vilivyofanywa na viongozi husika na linatoa pole kwa wauguzi waliopatwa na kadhia hii," amesema Mfalila.
No comments:
Post a Comment