Sunday, March 11

Maandamano mtandaoni yamwibua Cheyo


Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo amesema mabaraza ya vyama vya siasa yakitumika kikamilifu yanaweza kuondoa malalamiko ya wananchi na viongozi wa upinzani.
Amesema hayo leo Machi 11,2018 akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu vuguvugu la maandamano yaliyopangwa kufanyika Aprili 26,2018 yanayoratibiwa kupitia mitandao ya kijamii.
Cheyo amesema maandamano hayo ni uchochezi na uvunjifu wa amani na kwamba, mambo yanayolalamikiwa yangeweza kutatuliwa kupitia mabaraza hayo.
"Tusitake kufika hatua ya kuandamana barabarani ili kudai haki, Katiba mpya, Tume huru ya uchaguzi. Tukifikia huko amani iliyopo Tanzania tutashindwa kuipata tena na wananchi watakosa nchi nyingine yenye amani ya kukimbilia," amesema.
Cheyo amesema kama tatizo ni fedha kwa ajili ya mabaraza hayo kukutana, Rais John Magufuli anapaswa kutoa fedha kuyawezesha kufanya vikao.
"Siungi mkono hoja za kudai kuwepo mikutano ya hadhara hata kama ni kwa ajili ya kuongeza wanachama kama wanavyodai wengine, naamini kwa sasa mitando ya kijamii ina nguvu kuliko kitu chochote nchini," amesema Cheyo.
Amesema kabla ya kudai haki ya kuandamana, zipo nyingine wananchi wapaswa kuzipa kipaumbele zikiwemo haki ya kuishi, kupata maji safi na salama, elimu na afya.
"Hatuwezi kufika mahali tuseme nchi hii imepotea na hakuna demokrasia kisa tumekosa haki ya kuandamana, haki ya kufanya mikutano ya hadhara. Kila mtu alishuhudia mikutano ya kampeni za uchaguzi wa ubunge wa marudio katika majimbo ya Kinondoni na Siha ilivyogeuka sehemu ya kutukanana," amesema Cheyo.
"Kama kitu mnachokidai kiliweza kusababisha watu kugombana na askari hadi mauaji yakatokea hicho kitu hakitusaidii kama nchi," amesema.
Cheyo amesema yanayodaiwa kwa nguvu hayana faida na manufaa ya kila siku kwa sababu watu wanahitaji kupata wakati wa kulima na kuvuna.
"Hiyo mikutano iliyoshupaliwa sasa na kuhitajika kwa nguvu zote si kweli kwamba kila siku watakuwa barabarani kuhutubia wananchi, fedha tutatafuta saa ngapi, tutalima saa ngapi, hivyo ni vyema tutambue kila kitu kinachofanyika kupitia mambo ya siasa kisiwe kisingizio cha kusema nchi haina amani, haina uhuru," amesema Cheyo.
Amesema viongozi wa dini wanapaswa kuwa kiunganishi cha wananchi na viongozi wa vyama vya siasa na si kufanya kinyume cha hilo.

No comments:

Post a Comment