Sunday, March 11

Kila nchi ina wajihi, siha na tabia zake...

Kila nchi utakayoitembelea...
Kila taifa, huwa na taswira yake.
Juzi rafiki yangu alirejea toka Misri. Shughuli zake ni vichekesho (“standup comedy”) sanaa iliyo juu sana Uzunguni. Ucheshi wa kibunifu hauudhi sana watawala.
Chukua mchekeshaji maarufu wa Afrika Kusini – Trevor Noah.
Husema mengi sana katika onesho la dakika kumi tu.
Aliwahi kuelezea namna Mama yake mzazi alivyopigwa risasi. Kiherehere cha kukimbilia hospitali, na mdogo wake asiyeelewa kunanini. Utacheka hapo hapo ukigundua mengi kuhusu ughali na dhiki ya matibabu leo Afrika. Usipokuwa nazo utafariki tu.
Sasa jambo la kwanza alilosema rafiki yangu mchekeshaji ni namna Wamisri walivyo poa.
Akaonesha picha alizowapiga ngamia. Wachekeshaji sio?
Hatuwawezi.
Niliwahi kuishi Canada miaka ya Tisini; na baridi kali kule kiasi ukitema mate hugeuka barafu kabla hayajagusa ardhi! Hapo hapo Wacanada wamejenga mazingira kuhimili baridi. Magari yana minyororo ya chuma katika magurudumu, nyumba zenye vipasha joto sakafuni na mazuliani, nk.
Safari ni mwalimu
Nilipowasili mara ya kwanza Ulaya miaka ya Themanini nilishangazwa na sura za watu wasiojua kucheka ...hadharani. Kila mtu mbio mbio; hasemi na mwenzake. Vyombo vya usafiri vikishasimama tu- kila mtu, kimbilia kukitoa.
Utamaduni wa kila mtu na lwake, kutosemeshana, mbio kasi za duma. Upande mwingine hawa hawa huwa marafiki wa kweli mkijuana. Huenda wasikusemeshe njiani, lakini ukiwa na shida, kama mnafahamiana, Utamshukuru Mungu.
Marekani ya Kusini ni kinyume cha Ulaya. Joto, jua, kelele za muziki kila mahali. Kama tulivyo Waafrika (kadamnasini) uzungumzaji mkali. Humjui hakujui katika basi, mtasalimiana, mtajuliana hali, mtachapa “mastore.”
Kuna wakati nilirudi Tanzania na wageni wangu. Ilikuwa mara ya kwanza kwa mmoja wao kuwemka mguu Afrika...
Nikaulizwa :
“Mbona Watanzania wana macho mekundu sana?”
Zamani nikiwa mdogo nakumbuka tuliona fahari mtu akiwa na macho mekundu.
“Jeuri yule...usimchezee!”
Utoto huo.
Ukosefu wa maji mwilini na baadhi ya vitamin ni kati ya sababu macho kubadilika rangi. Watanzania (na Waafrika kijumla) tunapenda sana vitu vya ladha. Vyakula vyenye chumvi na pilipili nyingi. Vinywaji vyenye sukari sukari (soda) ni mifano michache. Juzi hapa London nilikaribishwa mlo wa jioni na dada mmoja wa Kiafrika. Ile salad (tango, karote na nyanya) zilinakshiwa kwa chumvi.
“Mbona chumvi katika Salad?”
“Ladha, Bw Freddy.”
“Lakini chumvi si iko katika nyama na mchuzi ?”
“Si umeona utamu kaka.”
Hapo ndipo lilipo jehanam dogo la afya zetu. Watu weusi sasa hivi (dunia nzima) wanakabiliwa sana na tatizo la figo. Wanawake wanapata mawe sehemu hizo. Wanaume athari huenda hadi uumeni (haja ndogo, tezi kibofu, urijali nk).
Kazi kuu ya figo ni kusafisha damu na tumbo. Kupiga deki mwili. Unapolijaza tumbo na vitu vyenye ladha tupu, kila siku, kila mara, unahatarisha sana afya ya figo. Ongeza sasa kama hunywi maji...(wanywa tu wakati wa kula au soda). Au hufanyi mazoezi ya viungo. Tusishangae kuona maisha yetu mafupi. Kutokunywa pombe na kusema soda, chai au kahawa hakuna maana figo zetu zinapona. Tujifunze kujipenda na kupenda uasilia. Gharama za matibabu huwa juu kuliko zile za vyakula vya afya.

No comments:

Post a Comment