Taarifa ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro iliyotolewa jana imeeleza kuwa Agosti 4, katika eneo la Gari Bovu, Kijiji cha Chamiwaleni wilayani hapo polisi walimkamata Abdallah Mbindimbi Abajani akiwa ana majeraha maeneo mbalimbali ya mwili wake akionekana kuwa alikuwa anaendelea kujitibu mwenyewe kwa kificho.
Alisema alipohojiwa kuhusiana na tuhuma zinazomkabili, alikubali na alionyesha dhamira ya kwenda kuonyesha ngome yao.
Alisema juzi katika mapori ya Kijiji cha Rungungu, mtuhumiwa huyo aliwaonyesha polisi ngome ya watuhumiwa wenzake aliokuwa anashirikiana nao kufanya uhalifu.
“Baada ya kukaribia eneo la tukio ulitokea upinzani mkali wa majibizano ya risasi jambo lililosababisha hata Abdallah Mbindimbi Abajani kujeruhiwa kwa risasi sehemu mbalimbali za mwili wake.”
Alisema kutokana na majibizano hayo, polisi waliwajeruhi wahalifu 12 ambao baadaye walifariki dunia, (akiwamo Abdallah) kwa nyakati tofauti wakipelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutokana na kuvuja damu nyingi zilizosababishwa na majereha ya risasi.
“Miili ya marehemu imehifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.”
Aliwataja watuhumiwa saba kati ya 13 waliopoteza maisha kuwa ni Hassani Ali Njame, Abdallah, Saidi Abdallah Kilindo, Abdulshakuru Mohamed Ubuguyu, Issa Mohamed Mseketu, Rajabu Thomas na Mohamed Ally Kadude Upolo.
“Miili 6 (sita) iliyobaki haikuweza kutambulika mara moja hivyo utambuzi utaendelea huko ilikohifadhiwa hospitalini.”
“Taarifa za utambuzi wa vielelezo vilivyopatikana eneo la tukio na utambuzi wa baadhi ya miili ya watuhumiwa waliofariki zinaonyesha kuwa walishiriki matukio ya uhalifu maeneo mbalimbali kama ifuatavyo:
“Kuua OC CID na watumishi wawili wa Idara ya Maliasili katika tukio la Jaribu Mpakani, Wilaya Kibiti. Kuua askari polisi wanane katika tukio la Mkengeni wilayani Kibiti.”
Alisema matukio mengine ni kuua trafiki wawili katika eneo la Bungu “B” wilayani Kibiti, kumuua diwani wa zamani CCM katika tukio la Kibwibwi wilayani Kibiti na kuua ofisa mtendaji, mwenyekiti wa mtaa na mkulima katika tukio la Kijiji cha Mangwi wilayani Kibiti.
No comments:
Post a Comment