Friday, August 11

NAIBU MEYA WA MANISPAA YA DODOMA JUMANNE NGEDE ATETEA NAFASI YAKE



Na Ramadhani Juma-Ofisi ya Mkurugenzi

NAIBU Meya wa Manispaa ya Dodoma aliyemaliza muda wake Jumanne Ngede amefanikiwa kutetea nafasi yake katika uchaguzi uliofanyika jana katika ukumbi wa Manispaa ya Dodoma ambapo wajumbe 56 walishiriki uchaguzi huo.

Katika uchaguzi huo Ngede ambaye ni Diwani wa Kata ya Chamwino kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) alishinda nafasi hiyo kwa kupata kura 47 dhidi ya mpinzani wake kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Samwel Mziba ambaye ni Diwani wa Kata ya Hazina aliyepata kura 9.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma ambaye ni Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Dodoma Mjini Godwin Kunambi alimtangaza rasmi Ngede kuwa Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma.

Baada ya kufanikiwa kutetea nafasi yake, Ngede aliwashukuru wajumbe kwa kumchagua kwa kura nyingi jambo linaonesha kuwa wana imani kubwa na utendaji wake na kwamba ataendelea kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa na kwa kushirikiana na Madiwani wote.

Kwa upande wake, mgombea aliyeshindwa Samweli Mziba aliwashukuru wajumbe na kumpongeza mshindi huku akidai uchaguzi umepita na sasa ni kuchapa kazi tu.
 Mgombea aliyeshinda nafasi ya Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumannne Ngede (CCM) akitoa neno kwa wajumbe mara baada ya kushinda nafasi hiyo kufuatia uchaguzi uliofanyika jana katika ukumbi wa Manispaa hiyo.
   Mgombea aliyeshindwa nafasi ya Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Samwel Mziba  (CHADEMA) akitoa neno kwa wajumbe mara baada ya matokeo kutangazwa kufuatia uchaguzi uliofanyika jana katika ukumbi wa Manispaa hiyo.

No comments:

Post a Comment