Friday, August 11

Utaratibu wa kuingiza, kutoa hela nchini wawekwa


Dar es Salaam. Wizara ya Fedha na Mipango imeandaa kanuni za taarifa za usafirishaji na uingizaji wa fedha taslimu kutoka na kwenda nje ya nchi ambapo wasafirishaji wa fedha taslimu na wasafiri wote wanaotoka au kuingia nchini, watatakiwa kutoa taarifa za fedha taslimu wanazosafirisha ikiwa fedha hizo zinalingana au zinazidi kiasi cha dola za Marekani  10,000.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku mbili ya maandalizi ya utekelezaji wa kanuni hizo, Kamishna na Mtendaji Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU),  Onesmo Makombe alisema utekelezaji wa kanuni hizo, pamoja na mambo mengine utaiwezesha nchi kuwa na takwimu za usafirishaji fedha taslimu.
“Takwimu hizo zitakazosaidia pamoja na mambo mengine kubaini vitendo vya kihalifu, kupunguza utoroshaji wa mitaji na kuhakikisha kuwa tunapunguza kama siyo kumaliza kabisa usafirishaji wa fedha zitokanazo na uhalifu na fedha kwa ajili ya kufadhili ugaidi,” alisema Makombe
Vilevile kanuni hizo zimeweka adhabu zitakazochukuliwa dhidi ya wale watakabainika kutaka kupita na fedha zinazolingana au zinazozidi kiwango kilichowekwa bila kutoa  taarifa au watakaotoa taarifa za uongo.
Alizitaja adhabu hizo kuwa ni pamoja na kukamatwa kwa fedha taslimu walizonazo na kuchukuliwa hatua nyingine za kisheria kama vile kufunguliwa mashtaka.
“Wahalifu pamoja na mambo mengine, wanapenda kusafiri na fedha taslimu kwani wanaogopa kutumia benki kutuma fedha kutokana na umakini unaoongezeka katika benki na udhaifu unaoweza kuwepo mipakani,”  alisema Makombe.
Kamishna huyo amewaasa washiriki wa warsha hiyo kutekeleza jukumu hilo  kwa uadilifu na uaminifu mkubwa  ili kuziba mianya yote ambayo wahalifu wanaweza kuitumia kutimiza kusudi lao ovu na kuhatarisha usalama wa nchi.

No comments:

Post a Comment