Lema alipata ajali hiyo wakati akirejea mjini Graz kutoka kwenye matembezi yake ya kawaida ya kuwatembelea jamaa na marafiki ambao wanaishi nje kidogo ya mji huo.
Spoti Mikiki imefanya mawasiliano na winga huyo ambaye amepandishwa kikosi cha kwanza cha timu hiyo mara baada ya kufanya vizuri akiwa na Kikosi B kwenye ligi ya vijana na kupewa mkataba wa miaka mitatu.
Mawasiliano hayo, yalilenga kufahamu hali yake kwa ujumla, chanzo cha ajili hiyo na walezi wake walipokeaje taarifa ya kupata kwake kwa ajili hiyo akiwa kwenye gari yake aina ya Volkswagen.
“Nilitoka mazoezini na kumaliza program zote za siku hiyo kwa maana ya mazoezi binafsi ambayo nayo nimekuwa nikifanya kila siku ili kuhakikisha na kuwa fiti mara dufu.
“Siku hiyo nilikuwa na ahadi ya kuwatembelea marafiki zangu ambao muda mrefu kidogo hatukuonana nje ya mji ninaoishi, nilikwenda salama kabisa na kukutana nao.
“Muda ulikuwa umesogea kidogo na giza lilikuwa limeingia baada ya maongezi marefu na kufurahi pamoja, nilianza safari ya kurejea nyumbani, sikuwa kabisa nimetumia kilevi cha aina yoyote,” anasema Lema.
Winga huyo ambaye alifunga mabao matatu kwenye michezo nane ya kikosi B kabla ya kusaini mkataba na kupandishwa, alisema ajali hiyo ilichangiwa na kuendesha kwake kwa mwendo kasi.
“Ninakiri nilikuwa spidi na kilichotokea kiukweli nilishindwa kudhibiti mwendo kasi ule na nikayumba kwa kugonga ukingo wa barabara na kupata mstuko ambao ulinifanya kupoteza fahamu na nilijitambua wakati nikiwa hospitali.
“Sikupata majeraha na unafuu wa huku ni kwamba kuna kamera mitaani ni rahisi kupata msaada kama kuna tatizo limetokea, ajali haina kinga cha kushukuru Mungu ni kwamba nimetoka nikiwa salama.
“Ilinichukua siku tatu ambazo niliwekwa chini ya usimamizi wa madaktari ambao walinifanyia vipimo vyote na kubaini sikuwa na tatizo lolote ambalo limesababishwa na ajali hiyo zaidi ya michubuko wa kawaida,” anasema chipukizi huyo.
Anaendelea: “Kosa nililofanya ni kuendesha gari kwa mwendo kasi, kwa kosa hilo nimeadhibiwa kutoendesha chombo chochote cha mwendo moto kwa maana ya kuanzia gari hadi pikipiki kwa miezi sita.”
Hata hivyo, Lema hakuonyesha kusikitika kuharibika vibaya kwa Volkswagen yake yenye thamani ya Sh94 millioni.
“Thamani ya uhai wangu ni kubwa kuliko gari ambayo haitamaniki tena,” alisema Lema.
Nyota huyo wa Tanzania, anasema atarejea kwenye program za timu yake baada ya wiki tatu ambazo amepewa za kuhakikisha anarejea kwenye hali yake ya kawaida.
“Mwanasaikolojia wa timu alikuja na tukaongea na dhani atakuwa alikuja kuona ni kwa namna gari ile ajali iliniathiri kisaikolojia ila sioni kama nimeathirika kwa namna yoyote.
“Pamoja na yote nimesikita kupata ajali hii kwa sababu imefanya kukaa nje ya uwanja kwa wiki tatu tena ambazo kama ningekuwa kwenye program za timu ina maana ningekuwa kwenye nafasi nzuri ya kupewa nafasi ya kucheza.
“Hakuna ubaya lakini kwa sababu kila kinachotokea huwa na sababu zake, naamnini nitarejea na kuendeleza mapambano ya kuwania nafasi kwenye kikosi cha kwanza,” anasema.
Lema hakusita kuishukuru Spoti Mikiki kwa kuwa karibu naye hata hivyo alitumia nafasi hiyo kuwaambia ndugu na jamaa na marafiki zake ambao wapo Tanzania kuwa anaendelea vizuri mara baada ya kupata matibabu ya michubuko aliyopata kwenye ajali hiyo.
No comments:
Post a Comment