Tuesday, April 3

Tumbili aiba mtoto na kutoroka naye India

macau monkeyHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Polisi nchini India wanamsaka tumbili mmoja ambaye aliiba mtoto na kutoroka naye katika jimbo la Orissa, mashariki mwa nchi hiyo.
Mwili wa mtoto huyo ulipatikana baadaye kwenye kisima.
Mamake mtoto huyo mvulana anasema alishuhudia kisa hicho kikitokea lakini hakuweza kumuokoa.
Jamaa wake aliupata mwili wa mvulana huyo kwenye kisima nyuma ya nyumba yao, siku moja baada ya mvulana huyo kuibwa na tumbili huyo.
Mnyama huyo alikuwa ameingia ndani ya nyumba ya familia hiyo na kumtwaa mtoto huyo.
Polisi wanasema kisa hicho ni cha kipekee sana, ingawa mara kwa mara tumbili hupatikana wakiharibu mali eneo hilo.
"Tunatumai kwamba tutafanikiwa kumkamata tumbili huyu katika kipindi cha wiki moja," afisa mmoja wa polisi kwa jina Pradhan ameambia BBC.
"Ingawa visa vya tumbili kuwashambulia binadamu au kuingia kwenye manyumba ya watu wakitafuta chakula ni vya kawaida, hiki ndicho kisa cha kwanza kwa tumbili kutoroka na mtoto," ameongeza.
Polisi wanashirikiana na watu wa jamii moja eneo hilo, ambao ni stadi wa kuwakamata tumbili.
Maafisa wa idara ya msitu wameambia BBC kwamba tumbili huyo aliingia kwenye nyumba ya familia hiyo Jumamosi asubuhi na kutoroka na mtoto huyo.
Daktari aliyeuchunguza mwili wa mvulana huyo anasema haukuwa na alama za majeraha.
"Inaonekana alifariki kutokana na kukosa hewa pengine kutokana na kuzama kwenye maji kisimani," amesema daktari huyo.
Wakazi wameambia wanahabari kwamba huenda tumbili huyo alimwangusha mtoto huyo akitoroka.

No comments:

Post a Comment