Tuesday, April 3

Wakimbizi waliokufa ajalini kuzikwa nchini



Ngara. Miili ya wakimbizi wanane raia wa Burundi waliopata ajali ya gari wilayani hapa Mkoa wa Kagera, Machi 29 mwaka huu wakitokea kambi za Nduta Wilaya ya Kibondo, Kigoma itazikwa leo (Jumatatu) eneo la Lumasi.
Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Michael Mtenjele alitoa taarifa hiyo jana kwa waandishi wa habari waliotaka kujua hatima ya miili ya marehemu hao iliyohifadhiwa Hospitali ya Nyamiaga.
Mtenjele alisema baada ya kufanyika taratibu za kimatibabu kwa majeruhi wa ajali hiyo, watendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Tawi la Ngara na Kibondo, wameomba ardhi ya kuhifadhi miili hiyo eneo la Lumasi ya Benako wilayani hapa.
“UNHCR ndiyo wanaratibu shughuli za mazishi ya miili hiyo, Serikali tunawapa ushirikiano wa kile wanachohitaji kwa mujibu wa sheria wala hatujapata tamko lolote kutoka Serikali ya Burundi kuhusu vifo hivyo,” alisema Mtenjele.
Katika ajali hiyo kulikuwa na msafara wa magari manane yenye wakimbizi 515, gari mojawapo lilifeli mfumo wa breki na kuligonga lingine kwa nyuma na kusababisha vifo vya watu wanane na majeruhi 95.
Mganga wa Hospitali ya Murugwanza, Remmy Andrew alisema majeruhi 22 wameruhusiwa na kupelekekwa kituo cha mapokezi kambi ya muda ya wakimbizi ya Lumasi.
Alisema majeruhi wanne wamepewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Bugando, Mwanza kwa kusafirishwa na UNHCR, hivyo kubakia majeruhi wanane wanaoendelea kupata matibabu.

No comments:

Post a Comment