Sunday, November 26

Wanawake bado wanatafuta tofauti ya mwanaume na ng’ombe


Kuna mambo yasiyofanana lakini huwezi kuyatofautisha’; unaweza kuisoma sentensi hiyo kadri utakavyo ili uilewe, lakini kuna mfano kwa ajili ya kukufunulia.
Ni hivi, ulishawahi kugundua kuwa hakuna tofauti kati ya mke wako kukwambia ‘Tunaondoka sasa hivi baba Ashura, namalizia kuvaa’ na wewe kumwambia ‘niko njiani mke wangu, nafika nyumbani sasa hivi’?.
Ni sentensi mbili tofauti kabisa, zisizofanana karibu kila kitu, kuanzia muundo hadi maana lakini linapokuja suala la mantiki huwezi kuzitofautisha kwa sababu ‘kuvaa kwa mwanamke’ ni mwaka mzima na ‘nakaribia nyumbani ya mwanaume’ ni sawa na miezi kumi na mbili kama sio siku 365.
Kingine kisichofanana lakini huwezi kutofautisha ni wale waliobahatika kuzaliwa katika familia zenye watu wenye kiwango cha juu cha elimu. Zile familia za kila unayemgusa alikuwa anafanya vizuri darasani, halafu kwa bahati mbaya ni wewe tu katika familia nzima ndiye uliyekuwa na ‘perfomance’ mbovu.
Kitu ambacho wote tunatakiwa tufahamu ni kwamba, unapokuwa mtoto wa hivi, familia nzima, hasa wazazi wako waliokuwa wanakulipia ada, walikuwa hawaoni tofauti kati yako na ng’ombe. Na hata kama wakiamua kuitafuta, hawatapata ya maana zaidi ya utofauti wa mapigo ya moyo— kwamba moyo wa ng’ombe hudunda mara 48 hadi 84 kwa dakika na wa kwako 60 hadi 100.
Sasa jicho ambalo wazazi humtazama mtoto ‘kilaza’ ndilo ambalo wake zetu hututazama katika nyakati za migongano.
Ni hivi; ulishawahi kupita kwenye mikwaruzano na mwenza wako. Mikwaruzano mizito kabisa yakupitisha kwenye mpaka wa ndoa na kutengana—halafu ghafla mwanamke akatamka; “Hutokuja kupata mwanamke atakayeweza kuishi na wewe.”
Ulishawahi kufikia hatua hiyo? Kama ndiyo, uliichukuliaje kauli ya mwenza wako. Ulidhani ni kwa sababu umri umekwenda au kwamba wanawake wanaotaka kuolewa wameisha duniani kwamba ukimuacha yeye utasota? Au labda uliichukulia kawaida tu?
Kama uliichukulia kawaida, ulikosea, ulitakiwa kuipa uzito kwa sababu ndani ya moyo wake, hakuwa anamaanisha vitu vyepesi namna kama vile ulivyovisikia. Alikuwa anazungumzia jinsi ambavyo wewe huna tofauti na ng’ombe.
Alikuwa anamaanisha kwamba, siku mtakayoachana, wanawake wote wanaokupenda sasa hivi na kudhani kuwa wewe ni binadamu, watapata nafasi ya kuishi na wewe, wataziona tabia zako na kugundua ukweli kuwa wewe ni sawa na ng’ombe dume kitabia, kwa hiyo hakuna atakayeweza kuvumilia kuishi na wewe.
Wanawake wanajua kuzungumza kwa mafumbo sana. Sikiliza mara mbili mbili kila wanachokwambia.

No comments:

Post a Comment