Wednesday, July 19

Siri ya Mlima Mbeya kushika mkia matokeo kidato cha sita yaanikwa





Dar es Salaam. Siri ya Shule ya Sekondari ya Mlima Mbeya kushika mkia katika matokeo ya mtihani wa kidato cha sita imewekwa hadharani na mkuu wa shule hiyo iliyoko mkoani Mbeya, Atuganile Bwile akisema baadhi ya wanafunzi walikuwa na nidhamu mbovu.
Katika matokeo yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Jumamosi iliyopita mjini Zanzibar, Mlima Mbeya ni miongoni mwa shule 10 zilizofanya vibaya.
Orodha hiyo inajumuisha shule za Chasasa ya Pemba, Kiembesamaki (Unguja), Mwenyeheri Anuarite (Dar es Salaam), Ben Bella (Unguja), Meta na Mlima Mbeya (Mbeya), Njombe (Njombe), Al-Ihsan Girls (Unguja), St Vincent (Tabora) na Hagafilo (Njombe).
Bwile alisema baadhi wanafunzi walikuwa watoro na wengine walikuwa wakichagua mada za kusoma akitoa mfano wa baadhi waliokuwa wakisoma Kemia ambao walimueleza mwalimu wao husika kwamba mada anayofundisha ni ngumu hivyo hawataijibia mtihani. “Nimehamia shule hii nina miezi mitatu tu sasa, hawa wanafunzi walishindikana. Walikuwa wakiingia darasani wanavyotaka, huku wakiwa wamenyoa viduku. Nililazimika kuwabadilisha kitabia baadhi yao ndiyo maana tukaweza kupata hata daraja la kwanza mwanafunzi mmoja,” alisema.
Alisema daraja la pili wamefaulu wanafunzi  watano, la tatu 29, la nne 28 na sifuri ziko sita tofauti na matokeo ya mwaka jana ambayo hayakuwa na mwanafunzi aliyepata daraja la kwanza.
Bwile alisema kingine kilichosababisha matokeo mabaya ni kuwa walipokaribia kufanya mitihani, wanafunzi walifanya vurugu baada ya wenzao watatu kusimamishwa masomo kutokana na utovu wa nidhamu wakidai kwamba wenzao wameonewa ilhali uamuzi huo ulifikiwa na kikao cha walimu. Alisema vurugu hizo zilisababisha polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatuliza.
Hata hivyo, ofisa mmoja wa idara ya elimu mkoani Mbeya alisema walimu wa shule hiyo wanafundisha chini ya kiwango.
Ofisa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema alishaenda shuleni hapo zaidi ya mara mbili na kubaini kiwango cha ufundishaji kipo chini na kushauri yafanyike marekebisho, ushauri ambao alisema haukuzingatiwa.
“Wanafunzi kutokuwa na nidhamu kumesababishwa na walimu wenyewe kwa kufundisha chini ya kiwango,” alisema.

No comments:

Post a Comment