Friday, April 27

‘Kuleni vyakula vya asili kujikinga na maradhi’


Mtaalamu asema wakazi wengi wa Zanzibar wameweka utaratibu wa kula nyama kila siku
Zanzibar. Wakazi wa visiwani Zanzibar wameshauriwa kupunguza matumizi ya ulaji wa nyama badala yake watumie vyakula vya asili ili kujikinga na maradhi ya saratani.
Ushauri huo umetolewa jana na mtaalamu wa magonjwa ya saratani kutoka Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja mjini Unguja, Dk Msafiri Marijani wakati akizungumza na gazeti hili.
Alisema maradhi ya saratani kwa namna moja au nyingine yanasababishwa na ulaji wa nyama uliokithiri jambo ambalo alitaja siyo zuri kiafya.
“Kwa sasa walio wengi hapa Zanzibar wameweka utaratibu kula nyama kila siku nyumbani kwao na kibaya zaidi watu wameacha vyakula vya asili ambavyo ni bora kwa afya,” alisema Dk Marijani.
Daktari huyo alitaja sababu nyingine za ugonjwa huo kuwa ni pamoja na uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe pamoja na kuacha kufanya mazoezi.
Kutokana na hali hiyo pia alishauri jamii kuacha tabia ya matumizi ya sigara na unywaji wa pombe lakini pia kujiwekea utaratibu mzuri wa kufanya mazoezi kila siku angalau kwa dakika 30.
Katika hatua nyingine; alisema Hospitali ya Mnazi Mmoja ina vifaa vya kisasa vya kugundua ugonjwa huo wa saratani katika hatua za awali kabisa.
“Kila kitu tunafanya wenyewe hapa kuhusu saratani mgonjwa anayepewa uhamisho (transfer)ni yule anayehitaji kupigwa mionzi tu ambao ndio tunawapeleka Tanzania bara,” alisema Dk Marijani.
Katibu wa jumuiya ya watu wanaoishi na ugonjwa huo, Ali Zubeir Juma alisema maradhi hayo yanaongezeka siku hadi siku kutokana na jamii kukataa kubadili utaratibu wa maisha yao.

No comments:

Post a Comment