Wednesday, August 2

Taasisi za serikali kuacha kutumia mkaa na kuni


Serikali imeanzisha mkakati wa kuzitaka rtaasisi zake kuacha kutumia mkaa na kuni kama njia ya kupambana na kupoteza misitu kutokana na ongezeko la ukataji ovyo miti.
Waziri wa Nchi Ofisi wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Januari Makamba, amesema jiji la Dar es Salaam pekee limekuwa likitumia wastani wa tani 500,000 ya mkaa kila mwaka huku kukiwa na uwezekano wa kiwango hicho kuongezeka kutokana na jiji hilo kuendelea kupanuka.
Waziri Makamba amesema iwapo hali hiyo itaachwa iendelea kama ilivyo taifa linaweza kutumbukia katika jangwa na hivyo kuvuruga pia shughuli nyingine za maendeleo.
“Kwa kutambua hilo Serikali inakusudia kuipa uhai kampeni yake ya kupiga marufuku matumizi ya mkaa na tunataka baadhi ya taasisi za umma kuanza kuachana na matumizi ya mkaa na kuhamia katika utumiaji wa gesi,” alisema.
Inakadiriwa kuwa kila mwaka Tanzania hupoteza ekari milioni moja kutokana na matumizi ya mkaa na kuni na kwamba kiwango hicho kinaweza kuongezeka kutokana na ongezeko la mahitaji ya huduma hiyo.
Kama sehemu ya kuzidisha ufahamu juu ya athari zitokanazo na ukataji wa miti, Serikali inakusudia kuandaa maonyesho maalumu yatayofanyika mwakani yakiwa na lengo la kuibua mbinu mbadala ya nishati ya mkaa.

No comments:

Post a Comment