Shahidi huyo wa kwanza wa upande wa mashtaka akiongozwa kutoa ushahidi wake na Wakili wa Serikali, Constantine Kakula aliyaeleza hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba alipokuwa akitoa ushahidi wa sampuli ya mkojo huo aliodai kuupokea Februari 8.
Alidai kuwa siku hiyo, Wema alipelekwa ofisini kwa Inspekta Wills na WP Mary na kwamba baada ya kufikishwa, alimfanyia usajili na kupewa lebo namba 321/2017.
Katika ushahidi huo ulioanza kutolewa saa 7:25 mchana hadi saa 8:54, Mulima alieleza kuwa walimpeleka kwa sababu walitaka apimwe mkojo na kwamba alitoa kontena maalumu na kumpatia WP Mary ambaye aliongozana na Wema kwenye vyoo ambako alitoa sampuli ya mkojo huo.
Shahidi huyo alidai baada ya Wema kutoa sampuli hiyo, ilipelekwa maabara ambako aliipokea na kuendelea na uchunguzi. Hatua ya kwanza ilikuwa ni kupata chembechembe za dawa za kulevya ndani ya mkojo wa Wema na kwamba baada ya uchunguzi, iligundulika kuna dawa za kulevya aina ya bangi.
Shahidi huyo alibainisha kuwa kitaalamu, bangi inaweza kuonekana kwenye mkojo kwa muda wa siku 20. Baada ya kuthibitisha hilo, aliandaa taarifa ya mchunguzi ambayo aliisaini yeye mwenyewe na ikathibitishwa na kaimu mkemia mkuu wa Serikali na kwamba aliisaini Februari 8.
Shahidi huyo aliiambia Mahakama kuwa anaweza kutambua taarifa hiyo kwa sababu ina saini yake, muhuri wa moto na namba ya maabara na akaomba kuitoa mahakamani kama kielelezo cha ushahidi.
Wakili Peter Kibatala anayemtetea Wema, alipinga akitaka ripoti hiyo isipokewe kwa sababu haijakidhi Kifungu cha 63 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, Sura ya 20 iliyofanyiwa marekebisho 2002.
Kibatala alidai kuwa kifungu hicho kinaeleza utaratibu wa kufanya uchunguzi wa kitabibu kwa mshtakiwa ambaye yupo chini ya ulinzi kuwa ni lazima polisi awasilishe maombi mahakamani.
“Kwa sababu hakukuwa na ombi wala amri kutoka mahakamani ni lazima ripoti hiyo ikataliwe,” alieleza Wakili Kibatala.
Pia alipinga ripoti hiyo isipokewe kwa sababu pia haijaambatanishwa na fomu namba DCEA 001.
Kutokana na hoja hizo za Kibatala, Kakula alidai fomu yenye namba 001 inatumiwa na Polisi wanapopeleka sampuli na fomu namba 009 ni taarifa ya mkemia na kwamba fomu moja haitegemei nyingine kwa kuwa zinaandaliwa na watu tofauti.
Kakula alidai kuwa sheria haijasema kama ni lazima muda wote maombi yapelekwe mahakamani na oda itoke ndipo mshtakiwa afanyiwe uchunguzi wa kitabibu, ila pale ambako mshtakiwa hataki, polisi wanaweza kufanya maombi mahakamani.
Kibatala alisisitiza kuwa kuchukua kipimo cha utabibu ni lazima Polisi aende mahakamani na kwamba ripoti haijakidhi vigezo.
Kutokana na ubishani huo wa kisheria, Hakimu Simba alitaka Mahakama ipewe nafasi ya kuzipitia nyaraka zinazobishaniwa na kesi imeahirishwa hadi Agosti 4, 2017.
No comments:
Post a Comment