Wednesday, August 2

Bomoabomoa yaikumba nyumba ya Sh1 bil


Fundi akiondoa mabati katika paa la moja ya

Fundi akiondoa mabati katika paa la moja ya nyumba ya mkazi wa  Mbezi Kibanda cha Mkaa, jijini Dar es Salaam,  Margaret Kawa ili kupisha upanuzi wa Barabara ya  Morogoro kuanzia Kimara hadi Kiluvya.  Picha na Emmanuel Herman 
Dar es Salaam. Kuna vilio vingi vya kupoteza mali kutokana na bomoabomoa inayoendelea kupisha ujenzi wa barabara ya Morogoro, lakini sikia cha cha familia hii. Hivi sasa familia hiyo iliyowekeza kwenye ujenzi wa zaidi ya Sh1 bilioni katika eneo la Mbezi-Kibanda cha Mkaa, Dar es Salaam imeanza kuvunja nyumba zake kutii agizo la Wakala wa Barabara (Tanroards) la kutaka wabomoe wenyewe kabla hawajabomolewa.
Familia hiyo ya Magreth Kawa, iliwekeza nyumba kubwa nne za makazi kwenye eneo moja zikiwa zimezungukwa na fremu za maduka hiyo ikiwa ni mbali ya madarasa mawili ambayo mwalimu huyo mstaafu alikuwa akiyatumia kufundishia watoto wa chekechea.
Licha ya kuwapo kwa kesi mahakamani, baadhi ya wakazi hao wanaendelea kuvunja nyumba zao kwa hiari wakihofia kupoteza mali zaidi ikiwa bomoabomoa ya Serikali itaanza.
Waandishi wetu walishuhudia baadhi ya watu wakitokwa na machozi, wakati wakiendelea na shughuli ya kuvunja nyumba zao ama wenyewe au kwa kutumia mafundi.
Simulizi ya familia
Akizungumza kwa huzuni, Magreth alisema alijenga nyumba hizo tangu mwaka 1992, akishirikiana na watoto wake na kwamba amelazimika kubomoa ili kuokoa baadhi ya mali kabla hawajavunjiwa na kuambulia patupu.
Wakati mazungumzo na familia hiyo yakiendelea, baadhi ya mafundi walikuwa wakiendelea kuvunja nyumba hizo ili kuokoa bati na vifaa vingine kama milango, mbao na vile vya ndani yakiwamo masinki.
Ilikuwa ni kama tupo msibani kwa sababu waliokuwa wamekaa pembeni kusubiri nyumba hizo zivunjwe walikuwa wameshika tama huku wengine wakibubujikwa machozi.
Kilichowashtua hadi kuanza kubomoa nyumba hizo ni hatua ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuwakatia umeme jambo lililowapa ishara kwamba suala la ubomoaji huo halikwepeki.
“Kabla ya kuanza ujenzi maeneo haya yalikuwa mashamba yetu, baadaye tukaanza kujenga kidogokidogo,” alisema mmoja wa watoto wa mama huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe.
Alisema awali, wakati wameanza ujenzi sheria ilikuwa inawataka wajenge umbali wa mita 60 kutoka usawa wa barabara jambo ambalo, walilitekeleza.
“Wakati tunaanza ujenzi hatukuwa kwenye hifadhi ya barabara, tulikuwa nje kabisa lakini sasa wamekuja na sheria mpya kwamba ni mita 120, hivyo nyumba zetu zote zimejikuta zipo kwenye hifadhi,” alisema.
Alisema walikamilisha uwekezaji kwenye eneo hilo miaka mitano iliyopita na kwamba muda huu ulikuwa wa kuanza angalau kupata faida.
“Familia yetu tunaishi kwa pamoja hivyo uwekezaji huu tumeufanya pamoja tukimsaidia mama yetu, zipo nyumba ambazo tulikuwa tunaishi na nyingine tumepangisha,” alisema.
Magreth alisema kinachowaumiza zaidi ni kutoambulia fidia ya aina yoyote kutokana na uwekezaji mkubwa walioufanya.
Alisema kwa kuwa hawakuwa wamejipanga, wamelazimika kuweka baadhi ya vyombo vyao kwa ndugu wakati wakitafakari watakavyoanza maisha mapya.
Kama ulidhani hicho ndicho kilio kikubwa pekee sikia na hiki cha mkazi wa Kimara Stop Over, Santand Kayu. Huyu tayari ameshavunja nyumba yake aliyoijenga kwa mkopo miaka minne iliyopita ikigharimu zaidi ya Sh120 milioni, fedha ambazo bado anaendelea kulipa.
“Nimevunja ili walau niokoe bati na vitu vingine, tunaendelea kusubiri kesi iliyo mahakamani,” alisema.
Alisema tathmini ya awali iliyokuwa imefanywa, wale waliojenga kabla ya barabara hiyo walitakiwa kulipwa fidia lakini tathmini mpya haijaainisha malipo ya fidia yoyote.
Simulizi ya wajane wawili
Tukiendelea kutembelea makazi yaliyowekewa alama ya X nyekundu na maandishi ‘Bomoa’ , waandishi wetu walifika katika nyumba ya vyumba sita iliyojengwa na Joyce Elias (70) akishirikiana na marehemu mumewe tangu mwaka 1994.
Nyumba hiyo inadaiwa kuwa na thamani ya zaidi ya Sh60 milioni lakini inatakiwa kuvunjwa.
Mwandishi wetu alifika katika nyumba hiyo juzi saa 10 jioni na kumkuta Joyce akiwa ameketi nje huku akitengeneza ufagio wa ‘chelewa’ kwa kutumia majani ya minazi iliyokauka.
Alionekana tofauti kabisa na wananchi wengine wa eneo hilo ambao wengi wao walikuwa ‘bize’ wakivunja nyumba zao. Alikaa tu kana kwamba hajui kinachoendelea huku pembeni yake wakiwapo watoto wawili ambao baadaye alisema ni wajukuu wake, hao walikuwa wakichambua mboga za majani, mara alimwagiza mmoja wao, “Rebecca mletee dada yako kiti.”
Baada ya kuketi, mwandishi wetu alimuuliza kuhusu bomoabomoa hiyo na mama huyo alijibu kwamba anajua kwamba nyumba yake inatakiwa kuvunjwa lakini haamini kama hilo litatokea hivyo anasubiri mpaka dakika ya mwisho maana hana pa kwenda huku akiwa na mgonjwa ndani na wajukuu watano ambao wote wanamtegemea.
“Leo wananiambia nihame hapa nitakwenda wapi? Ndani nina mgonjwa mdogo wangu.”
Alisema mdogo wake huyo, Rose Elias (68) ambaye pia ni mjane, baada ya kupata taarifa za kubomolewa kwa nyumba yao amepooza.
“Alikuwa anaumwa muda mrefu hili suala la kubomolewa ndiyo limemmaliza zaidi sasa hivi kapooza hawezi kutembea,” alisema.
Akieleza ilivyokuwa mpaka mdogo wake kupooza, Joyce alisema siku maofisa wa Tanroads walipoenda kuweka alama ya kuvunjiwa nyumba alikuwa amekaa nje na mdogo wake huyo, pamoja na mmoja wa wajukuu wake, Rebecca.
“Tukiwa hapa nje tukashuhudia wakiweka alama kwenye nyumba. Tuliamini wataishia nyumba za juu mara tukaona wamefika hadi kwenye nyumba yangu na kuweka alama, mdogo wangu alikuwa amekaa hapa (akionyesha kwa mikono) nikasikia akisema ‘Ha! Ha! Ha Rebeca tutakwenda wapi mjukuu wangu!’” alimnukuu.
Alisema baada ya kusema hivyo alianguka hivyo wakalazimika kumpepea, ingawa baadaye alipata nafuu, alisema ilipofika usiku hali ilibadilika tena akashindwa kuongea wala kutembea na alipopelekwa hospitali ikaonekana amepooza.
“Ndo hivyo ilivyokuwa mjukuu wangu kwa hiyo bibi yako yupo tu ndani kalala, nitakupeleka ukamuone, sasa hawa wote wananiangalia mimi, mgonjwa ana wajukuu zake hapa ambao ni watano baba yao aliwatelekeza na mama yao alishafariki kwa hiyo naishi nao,” alisema.
Joyce alisema nyumba yake ilikuwa na wapangaji watano wote wameondoka na wengine bila kulipa madeni aliyokuwa akiwadai na fedha alizokuwa nazo zimetumika kumtibu mdogo wake na kumzika mtoto wa mdogo wake ambaye alifariki wiki mbili zilizopita kwa maradhi mengine ambayo alisema hayahusiani na bomoabomoa hiyo.
Baadhi ya majirani wa Joyce walisema mjane huyo anaishi maisha magumu, “Ile familia kiukweli ina wakati mgumu mno, tunafahamu kuna mwingine alipooza ghafla tu baada ya kupata mshtuko” alisema Rehema Kihondo.     

No comments:

Post a Comment