Wednesday, July 26

TANZANIA YAJIPANGA KUISHAWISHI UINGEREZA, FURSA ZA UWEKEZAJI NISHATI, MADINI NCHINI: BALOZI MIGIRO, DKT. PALLANYO, WATAALAM WA WIZARA WAKUTANA


Na Veronica Simba – Dodoma
Kufuatia Kongamano kubwa la Uwekezaji linalotarajiwa kufanyika nchini Uingereza, mwezi Septemba mwaka huu, Balozi wa Tanzania nchini humo, Dkt. Asha-Rose Migiro amekutana na wataalam wa Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi zake, wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo na kujadili fursa za uwekezaji nchini katika sekta husika.
Katika kikao hicho kilichofanyika Makao Makuu ya Wizara mjini Dodoma, Julai 24 mwaka huu, Balozi Migiro, alisema kuwa Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza umejipanga kulitumia vema kongamano hilo ambapo watanadi fursa za uwekezaji katika sekta zote muhimu nchini, zikiwemo za nishati na madini.
“Ni kwa sababu hiyo, nimeona nifike hapa ili nikutane nanyi, tujadili kuhusu fursa za uwekezaji hapa nchini katika sekta za nishati na madini ili tuweze kuzinadi wakati wa kongamano hilo,” alisema Balozi Migiro.
Akifungua majadiliano baina ya wataalam hao na Balozi Migiro, Naibu Katibu Mkuu Pallangyo, alibainisha kuwa zipo fursa nyingi za uwekezaji hapa nchini, katika sekta za nishati na madini na kupongeza hatua ya Balozi Migiro kudhamiria kuzinadi fursa hizo kwa wawekezaji nchini Uingereza.
Aidha, kwa upande wa sekta ya nishati, Dkt. Pallangyo alimwomba Balozi Migiro kupeleka maombi kwa Serikali za Uingereza na Ireland kusaidia miradi ya usambazaji umeme vijijini inayoendelea nchini kote.
Akizungumzia fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ndogo ya umeme, Mhandisi Nishati, Christopher Bitesigirwe alibainisha kuwa mpango wa serikali ni kuzalisha umeme hadi kufikia megawati 5000 ifikapo mwaka 2020 hivyo wawekezaji makini wanaendelea kukaribishwa.
Mhandisi Bitesigirwe alieleza kuwa, vyanzo vilivyoainishwa kwenye Mpango Kabambe wa Uendelezaji wa Sekta Ndogo ya Umeme ni pamoja na gesi asilia, maji, makaa ya mawe na nishati jadidifu (jua, upepo, jotoardhi na tungamotaka).
Kwa upande wa miradi ya usafirishaji wa umeme, alitaja fursa zilizopo kuwa ni pamoja Mradi wa kusafirisha umeme kuanzia Mbeya hadi Nyakanazi (North West transmission line) wa kilovoti 400, Iringa hadi Mbeya (KV 400), Chalinze hadi Dodoma (KV 400) na SomangaFungu hadi Kinyerezi (KV 400).
Vilevile, Mhandisi Bitesigirwe alitaja fursa iliyopo katika Miradi ya Usambazaji Umeme kuwa ni uboreshaji wa miundombinu ya usambazaji umeme.
Naye Mjiolojia Mkuu kutoka Idara ya Nishati, Habass Ngulilapi, alimweleza Balozi Migiro kuwa fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ndogo ya Petroli ni utafiti wa gesi asilia pamoja na mafuta unaoendelea nchini.
“Hadi sasa mafuta hayajagunduliwa nchini lakini kiasi cha futi za ujazo trilioni 10 za gesi asilia, kimegunduliwa katika maeneo ya mabonde ya nchi kavu,” alisema Ngulilapi.
Aliongeza kuwa, hadi kufikia mwezi Aprili 2017 kiasi cha gesi asilia kilichogunduliwa katika maeneo ya mabonde ya nchi kavu na katika kina cha maji mafupi na marefu ni futi za ujazo trilioni 57.25.
Kwa upande wake, Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi David Mulabwa, akizungumzia fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya madini, aliitaja miradi ya uongezaji thamani madini ya aina mbalimbali hapa nchini.
Mhandisi Mulabwa alibainisha kuwa, Mitambo ya kuchenjulia madini ya metali inahitajika sana kwa sasa hapa nchini ili kuwezesha kuchenjua madini hayo nchini pasipo kuyasafirisha nchi za nje, kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.
“Tayari wapo wawekezaji mbalimbali ambao wameonesha nia kuwekeza nchini kwa kuleta mitambo hiyo lakini kulingana na uhitaji na umuhimu wake, serikali bado inakaribisha wawekezaji wengine mbalimbali wenye nia ya dhati, waje kuwekeza katika eneo hilo,” alifafanua.
Aidha, Mhandisi Mulabwa, alibainisha fursa nyingine ya uwekezaji iliyopo katika sekta ya madini kuwa ni kuongeza thamani mawe mbalimbali ya vito kwa kuyakata na kuyang’arisha.
Akifafanua zaidi, alieleza kuwa, kuanzisha viwanda vya kutengeneza mapambo mbalimbali yanayotokana na madini ya vito na metali hapa nchini, ni fursa adhimu ambapo Serikali inawakaribisha wawekezaji makini kuja kuwekeza katika sekta hiyo.
Kaimu Meneja wa Uwekezaji kutoka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Nsalu Nzowa, alimweleza Balozi Migiro kuwa, fursa zilizopo kupitia shirika hilo ni kuendeleza Mradi wa kuchimba madini ya dhahabu wa Buhemba ambao ulikuwa ukitekelezwa kwa ubia kati ya Jeshi la Tanzania na la Afrika ya Kusini, na baadaye kusimamishwa.
Vilevile, alitaja fursa nyingine ya uwekezaji kuwa ni uchimbaji wa makaa ya mawe kwa ajili ya matumizi katika viwanda vya saruji pamoja na matumizi mengine mbalimbali.
Kwa upande wa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kijiolojia, Maruvuko Msechu, alimweleza Balozi Migiro kuwa Wakala huo unaendesha uchunguzi na tafiti mbalimbali za kijiolojia, ambazo zinahitaji ushirikiano kutoka kwa wadau mbalimbali.
Naye Mkurugenzi wa Kanzidata wa GST, Yokbeth Myumbilwa, alieleza kuwa, wawekezaji wanashauriwa kutembelea Tovuti ya Wakala huo ili kujipatia maelezo kuhusu tafiti mbalimbali zilizofanywa na Wakala zitakazowasaidia kupata uelewa wa aina mbalimbali za madini yanayopatikana nchini pamoja na maeneo yanakopatikana.
 












Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, anayeshughulikia masuala ya Nishati, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (kulia) akiwa katika kikao na Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Dkt. Asha-Rose Migiro (kushoto), Makao Makuu ya Wizara mjini Dodoma Julai 24, 2017. Wengine pichani ni wataalam wa Wizara na Taasisi zake walioshiriki kikao hicho.
 








Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, anayeshughulikia Nishati, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (katikati), akiongoza kikao cha wataalam wa Wizara pamoja na Taasisi zake na Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Dkt. Asha Rose Migiro (kushoto kwa Naibu Katibu Mkuu.)
 Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Dkt. Asha Rose Migiro (mwenye Koti la Pinki) na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia masuala ya Nishati, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (kulia kwa Balozi), wakiwa katika picha ya pamoja na wataalam wa Wizara pamoja na Taasisi zake, Makao Makuu ya Wizara, mjini Dodoma.
 















Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, anayeshughulikia Nishati, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (kulia), akimkabidhi Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Dkt. Asha-Rose Migiro, Kitabu cha Mpango Kabambe wa Uendelezaji Sekta Ndogo ya Umeme (Power System Master Plan). Wanaoshuhudia ni wataalam wa Wizara pamoja na Taasisi zake.
 
 















Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (kushoto), akiagana na Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Dkt. Asha-Rose Migiro (kulia), baada ya kikao baina yao Makao Makuu ya Wizara mjini Dodoma, Julai 24 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment