Wito huu wa Rais unaweza kuwa sehemu ya suluhisho la mimba kwa wanafunzi wa kike ila sio suluhisho bora kwa ustawi wa mtoto wa kike katika nyanja ya elimu.
Kwa maoni yangu, ni vyema tukajikita katika kutazama mzizi wa tatizo na kuweza kuondoa tatizo katika mzizi ili lisiendelee kujirudia badala ya kuishia kuangalia matokeo ambayo ni mimba yenyewe na kuishia kumhukumu mwanafunzi huyu kwa kumnyima elimu.
Natambua ya kuwa watu wengi wanadhani mwanafunzi kupata mimba ni suala la mwanafunzi husika kuwa mhuni tu ama tabia ya wanafunzi wa kike kupenda ngono.
Aina ya mawazo haya yanatokana na dhana za kibepari ambazo huaminisha watu ya kuwa tatizo la mtu husika ni tatizo lake mwenyewe na si tatizo la mfumo husika. Hapa ndipo utasikia unaambiwa ya kuwa mtu ni masikini kwa kuwa hajasoma, hajajiajiri, amelogwa, sio mchapa kazi na mengine mengi.
Aina hii ya mawazo tunayasikia kila siku kwa kuwa ubepari unaamini katika dhana ya ubinafsi na si dhana nzima ya jamii. Hali hii ndio inayotukumba katika hili la mimba za wanafunzi tunafikiri ya kuwa hili ni tatizo la watoto wa kike kwa kuwa hawajiheshimu, hawapendi masomo, wana tamaa ya ngono, pesa, wakaidi, hawana maadili na mengine mengi.
Kama ingalikuwa tatizo la mimba za wanafunzi ni lao moja kwa moja ama sababu kama hizo nilizotaja hapo juu zenye mrengo wa kibepari, basi kuwafukuza shule ingekuwa suluhisho.
Kwa mtizamo wangu mimba kwa wanafunzi wa shule sio tatizo binafsi tu bali ni tatizo la kimfumo linalochangiwa kwa asilimia kubwa sana na mazingira.
Natambua dhana ya mazingira ni pana hivyo ntatumia nadharia ya Human Ecology kueleza maana ya mazingira katika muktadha huu.
Nadharia ya Human Ecology inasisitiza ya kuwa mazingira ya asili ama yale ya kutengenezwa na binadamu huchangia mabadiliko ya tabia ya mtu husika. Kwa mantiki hii, mazingira yanaweza kuwa yale yaliyotengenezwa na binadamu, mazingira ya asili na mazingira ya kijamii tamaduni ambayo mtu husika hupatikana.
Nadharia hii inatuonyesha wazi ya kuwa tabia ya mtu yeyete huchangiwa na mwingiliano alionao na mazingira yake. Kwa kusisitiza zaidi vile tunavyoona tabia za watu leo hii ndio mwingiliano alionao na mazingira yake ya asili ama yale ya kutengenezwa na mwanadamu mwenyewe.
Labda nitoe mfano kidogo. Leo hii urembo na utanashati unatafsiri tofauti kutokana na mazingira ya sasa. Kwa wanawake ili waonekane warembo lazima watinde nyusi, wapake vipodozi, waweke nywele bandia na kuvaa mavazi tunayodhani ndiyo  ya kisasa.
Kwa wanaume, lazima uvae suruali za kubana mithili ya zile za kike, ushushe suruali nusu makalio, unyoe kiduku, kujichubua kidogo, kuvaa viatu bila soksi nakadhalika.
Hiyo mifano hapo juu inatoa taswira ya namna mazingira yetu yanaweza kuwa na nguvu kubwa ya ushawishi kiasi cha kukufanya utende bila kutumia utashi kwani usipofanya utaonekana wa kale hivyo ili kuendana na mazingira binadamu aliyoyatengeneza lazima ufanye kawa wao ili ufanane nao.
Suala la mimba za wanafunzi ni tunda la mazingira wanayoishi wanafunzi wetu hawa. Na kama tunataka kutatua tatizo hili ni vyema tuanze na kurekebisha mazingira yale ambayo si rafiki kwa wanafunzi wa kike ili kuondoa ama kupunguza kabisa tatizo la mimba za wanafunzi angali wako shuleni.
Hebu tutafakari kidogo, je, watoto wa kike kwanini hupata mimba nini hasa huwa kichocheo?
Kama nilivyosema hapo awali, wanafunzi hawa wa kike huishi katika mazingira aidha yaliyo rafiki ama yasio rafiki kwao. Hapa nitapenda kuangalia mambo kama umbali kufika shuleni, aina ya elimu inayotolewa shuleni, adhabu zitolewazo shuleni, mahitaji muhimu ya wanafunzi shuleni, umasikini, kukosa mlo wawapo shuleni, ukosefu wa vyumba vya kulala kwa wanafunzi watokao mbali, malezi hafifu, talaka, malezi kutokuwa ya jamii nzima, ombwe la maadili, elimu kutokuwa na mvuto, elimu isiyoleta matumaini ya ajira, tamaduni, siasa, ufisadi na mengine mengi.
Tunapoamua kuwahukumu wanafunzi kwa kuwanyima fursa ya kusoma ni kana kwamba tunasema wanafunzi hawa wanaishi katika ulimwengu wao peke yao na hili ni kosa lao binafsi na si kosa la mfumo wala mazingira.
Suluhisho la kweli katika vita dhidi ya mimba za wanafunzi ni kupambana na mazingira yanayowakumba wanafunzi wa kike badala ya kuendelea kuwakandamiza kwa kuwanyima haki ya kukosa elimu.
Endapo wanafunzi wa kike waliojifungua watakosa elimu ni dhahiri ya kuwa mzunguko wa umasikini utaendelea na kuongeza idadi ya wanawake waliokosa elimu na hivyo kuongeza wigo za tofauti ya kielimu baina ya jinsia hizi mbili.
Nihitimishe kwa kusema, makatazo pekee si suluhisho muhimu katika vita hii dhidi ya mimba za wanafunzi, bila kuyarekebisha mazingira yote yanayopelekea kuwepo kwa mimba za wanafunzi. Ni vyema sasa wizara ya elimu na idara zake husika ikafanya utafiti wa kina kugundua changamoto za kimazingira, binafsi na za kisaikolojia ili kuweza kuja na mbinu mbadala itakayokuwa na tija zaidi kwa watoto wa kike ili mapambano yawe ya kisayansi zaidi.
Mwandishi wa Makala hii ni mtaalamu wa Sayansi ya Jamii. Anapatikana kwa baruapepe; j_mulikuza2000@yahoo.com na simu +255 786 946 931