Wednesday, July 26

Hatima ya viongozi 51 wa Chadema kujulikana leo


VIONGOZI na wafuasi 51 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambao wameendelea kusota kwa siku 18 kwenye Gereza la Biharamulo mkoani Kagera kutokana na kunyimwa dhamana na Mahakama ya Wilaya ya Chato, hatma yao ikajulikana leo.

Ni baada ya mahakama hiyo kupokea hoja za upande wa mashtaka na utetezi ambao unaiomba mahakama kuondoa zuio la kutopewa dhamana ambalo liliwekwa na Mwendesha Mashtaka, Semen Nzigo.

Viongozi na wafuasi hao walikamatwa na Jeshi la Polisi wilayani hapa Julai 7, mwaka huu wakiwa kwenye kikao cha ndani kilichowahusisha viongozi wa Chadema mkoa, wilaya na Kata ya Muganza, ambapo walifunguliwa mashtaka ya kufanya mkusanyiko bila kuwa na kibali.

Baada ya pande hizo kuwasilisha hoja zao juzi, Hakimu wa Mahakama hiyo, Jovith Kato, alisema atatoa uamuzi wa mapingamizi hayo kesho, iwapo washtakiwa wapewe dhamana au waendelee kubaki mahabusu.

Wakizungumza nje ya mahakama, mawakili wa upande utetezi, John Edwar na Siwale Isambi, walisema wanatarajia mahakama itatenda haki kwa kuwapa dhamana kabla ya kesi ya msingi haijasikilizwa.

“Tunashukuru, mahakama imesema itatoa uamuzi wake keshokutwa (leo) iwapo wateja wetu wapewe dhamana au la...ila ni matumaini yetu makubwa kuwa zuio la upande wa mashtaka litaondolewa,” alisema Edward.

Baadhi ya viongozi walioko gerezani ni Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Geita, Phabian Mahenge, Katibu wa Chadema mkoa huo, Sudy Tuganyala, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee mkoa, Vitus Makoye na Mwenyekiti wa Bavicha mkoa huo, Neema Chozaile.

Wengine ni Katibu wa Wilaya ya Chato, Mange Ludomya, Kaimu Mwenyekiti Wilaya ya Chato, Uhuru Selemani, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa wilaya hiyo, Meshark Tulasheshe na Katibu Mwenezi Kata ya Muganza, Marko Maduka.

Hata hivyo, wakati mahakama hiyo ikitoa tarehe ya uamuzi wa pingamizi hilo, washtakiwa wote hawakuwapo mahakamani.

No comments:

Post a Comment