Hakuna mtu anapanga kushindwa kwenye mradi anaouanzisha bali kupuuza misingi ya biashara ndiko husababisha anguko. Mjasiriamali ambaye kila wakati anafuata misingi na taratibu za biashara kwa maslahi ya biashara yake huepuka changamoto hii.
Mjasiriamali anayezingatia kanuni hulifahamu vyema soko la biashara yake. Huepuka kuanzisha biashara ambayo bidhaa zake hazina soko.
Kabla ya kuanza biashara, mjasiriamali makini anatakiwa afanye utafiti na kujiridhisha kama kuna soko la kutosha baada ya kutambua bidhaa inayohitajika.
Mjasiriamali huyu pia huepuka gharama kubwa za maisha yake binafsi. Kufanikiwa katika hili huhakikisha ana wafanyakazi wanaohitajika kutoa huduma za msingi kulingana na ukubwa wa biashara na kuzingatia maeneo mengine kama hayo.
Mjasiriamali makini hutangaza bishara yake. Hutengeneza nembo makini na imara sokoni. Wanaoshindwa kwenye kipengele hiki hukosa wateja na kumaanisha mwisho wa biashara. Hawa huanguka kwa sababu huridhika kwa kuwa na biashara bila kufanya matangazo makini.
Mteja ni mfalme. Ukishindwa kumthamini utampoteza. Kinachomtofautisha mjasiriamali makini na anayebahatisha ni umakini katika kipengele hiki. Wajasiriamali wengi hawana huduma nzuri kwa wateja wao hivyo kwa muda mfupi tu huanza kukimbiwa na kwenda kwa washindani wao.
Wanakokimbilia ndiko aliko mjasiriamali anayejua wajibu wake kwa wanaomuweka mjini. Huyu hawezi kufunga virago na kuhama mji. Ataendelea kuwepo huku akiongeza idadi ya wateja.
Biashara ni tofauti na mmiliki wake. Hii inamaanisha haina uhusiano wowote na familia au rafiki zako. Inapotokea mjasiriamali akaruhusu marafiki au familia yake kufanya maamuzi katika biashara husababisha iyumbe hata kufa kabisa.
Kufanikisha jambo lolote unahitaji elimu kulihusu. Kama ilivyo kwenye maeneo mengine, huwezi kuwa daktari kwa mfano bila kuwa taaluma hiyo. Mjasiriamali makini huhakikisha ana elimu ya kutosha kuendesha biashara yake kwa kutambua kwamba kutofanya hivyo husababisha kudorora sokoni.
Kila baada ya muda Fulani, mjasiriamali makini anatakiwa kuhudhuria mafuzo ili kukumbushwa misingi ya uendeshaji biashara na mbinu mpya za kuliteka soko zilizopo. Bahati mbaya wajasiriamali wengi wana dhana kuwa biashara haihitaji elimu, ni kuuza na kupata hela ndiyo maana biashara nyingi zinakufa jambo ambalo halitokei kwa wachache waliotulia.
Kuepuka pupa ni sifa nyingine ya mafanikio. unaweza kuwa na mawazo mengi ya kufanya biashara ingawa unatakiwa kulizingatia moja au machache ambayo una uwezo nayo kwa misingi ya elimu, usimamizi, uzoefu, masoko na fedha.
Hairuhusiwi kuvamia biashara nyingi kwa wakati mmoja wakati huna uwezo nazo kwani husababisha kuanguka kibiashara. Jambo hili huepukwa kwa umakini na mjasiriamali makini.
Kukosea maamuzi katika kuanzisha na kuendesha biashara ni sababu kubwa ya kushindwa sokoni. Walio makini huwa makini kuchagua biashara ya kuanzisha, huzingatia ubora wa wafanyakazi na bidhaa husika.
Wengi ambao biashara zao hishia njiani ni wale wanaoshindwa kutimiza ahadi. Kutumia nguvu nyingi kutangaza biashara kwa ahadi za uongo ambazo huzitekelezeki ni kujinyonga kibiashara. Wateja watakuwa na matarajio ya kupata ulicho ahidi na ukishindwa kutimiza matarajio yao watakimbia. Mjasiriamali makini huahidi vitu anavyoweza kuvitekeleza kwa ufanisi.
Kama kuna kitu kinapaswa kuepukwa basi ni kufanya kila kitu mwenyewe. Kumiliki biashara na mipango ya kupata faida hakumaanishi ufanye kila kitu mwenyewe kwani unahitaji wataalamu wengine kukusaidia.
No comments:
Post a Comment