Thursday, November 23

Mgombea Chadema afutiwa kesi, akamatwa na polisi

Mgombea udiwani wa Kata ya Mhandu (Chadema),
Mgombea udiwani wa Kata ya Mhandu (Chadema), jijini Mwanza, Godfrey Misana. 
Mwanza. Mgombea udiwani wa Kata ya Mhandu (Chadema), jijini Mwanza, Godfrey Misana, meneja wake wa kampeni, Charles Chinchibela na wenzao wawili, wamejikuta wakiishia mikononi mwa polisi muda mfupi baada ya kufutiwa kesi ya kujeruhi.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza leo Alhamisi Novemba 23,2017 iliwafutia kesi washtakiwa na baadaye walikamatwa na polisi.
Mbali ya Misana na Chinchibela, wengine katika shauri hilo ni Dominick Izengo na Ibeneza Mathew.
Hata hivyo, Mathew hakuhudhuria mahakamani kutokana na taarifa zilizowasilishwa na mdhamini wake, William Victor kuwa anaumwa.
Mdhamini huyo ameshikiliwa na polisi kwa kushindwa kuhakikisha mshtakiwa anahudhuria mahakamani.
Awali, Hakimu Mkazi, Ainawe Moshi aliwaachia huru washtakiwa katika shauri namba 540/2017 la kumjeruhi meneja kampeni wa CCM katika kata hiyo, Thomas Warioba iliyokuwa ikiwakabili.
Hakimu ametoa uamuzi huo baada ya upande wa Jamhuri kupitia wakili Castus Ndamugoba kuwasilisha ombi la kuondoa shauri hilo mahakamani.

Wakili Ndamugoba amewasilisha ombi hilo akitumia kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai na Marejeo yake ya mwaka 2002 inayotoa fursa kwa upande wa Jamhuri kuondoa shauri mahakamani wakati wowote lakini hakizuii washtakiwa kukamatwa tena.
Washtakiwa walikuwa wakidaiwa kumshambulia Warioba katika tukio lililotokea Novemba 14,2017.  
Polisi waliowakamata washtakiwa wamekataa kusema lolote kwa maelezo kuwa wao si wasemaji.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Faustine Shilogile  hajapatikana kuzungumzia suala hilo baada ya waandishi wa Mwananchi waliofika ofisini kwake kuelezwa kuwa yuko kwenye kikao.

No comments:

Post a Comment