Thursday, November 23

Chadema yatoa tamko mgombea kuzuiwa kufanya kampeni


Dar es Salaam. Chama cha Chadema kimesema kimetii agizo la kutoendelea na kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata ya Saranga ili kumlinda mgombea wake, Eprahim Kinyafu kutoenguliwa katika kinyang’anyiro hicho.
Katibu wa Chadema Kanda ya Pwani, Casmir Mabina akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Novemba 23,2017 amesema kuna kila dalili za kumuondoa Kinyafu katika uchaguzi huo na kwamba, kumzuia kufanya kampeni ni njia mojawapo.
Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Novemba 23,2017 msimamizi msaidizi wa uchaguzi ambaye ni ofisa mtendaji wa Kata ya Saranga, Dandasi Kijo amesema Kinyafu amewekewa pingamizi la kutoendelea na kampeni baada ya kukiuka masharti ya kampeni.
"Uwezo tunao wa kuendelea na kampeni kutokana makosa yaliyofanyika katika mchakato wa kutuzuia lakini tumeona si busara kufanya hivyo kutokana na viashiria vilivyopo vya kutaka kumuondoa kabisa Kinyafu katika uchaguzi huu,” amesema Mabina.
Amesema, "Tumeona ni vyema tukatii ili tusiingie katika mtego ambao utasababisha wakazi wa Saranga kukosa mwakilishi bora na makini katika kusimamia kero zao."
Mabina amedai mchakato wa kuzuia kampeni za Chadema umefanyika kimakosa na mamlaka husika zina taarifa, hivyo wao kuendelea na kampeni ni sawa na kuingia kujimaliza.
Kwa upande wake, Kinyafu amewataka wakazi wa Saranga  kujitokeza kwa wingi Novemba 26,2017 kupiga kura ili Chadema ishinde.
"Hata tusipopiga kampeni wana Saranga wanajua nini cha kufanya. Wasishtushwe na pingamizi za kuzuia Chadema kufanya kampeni kwa siku zilizobakia," amesema  Kinyafu.
Wakati huohuo, Chadema imesema imeandika barua Tume ya Taifa ya Uchaguzi  (NEC), wakiomba kubadilishwa msimamizi wa uchaguzi John Kayombo ikidai amekiuka utaratibu wa maadili ya utumishi wa umma.
Pia, imeandika barua kwa Manispaa  ya Ubungo wakiomba wabadilishiwe msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa Halmashauri ya Ubungo.
Mabina amesema wamefikia uamuzi huo baada ya Kayombo kuonyesha wazi kuwa yupo upande wa CCM akimpigia kampeni kwa njia ya mitandao ya kijamii mgombea wa chama hicho.
"Hatuna imani na Kayombo kutokana na mwenendo wake si mzuri na amekuwa akichukua picha za kampeni ya mgombea wa CCM kisha kuzisambaza katika mitandao ya kijamii ikiwamo makundi ya WhatsApp," amesema Mabina.
Amesema, "Huyu, hatumtaki asimamie uchaguzi huu. Hii ngoma ipo uwanjani huyu refa hatufai atavuruga mchezo kutokana na tabia ya kufanya kampeni kimyakimya."
Kuhusu mtendaji wa Saranga, Kijo amesema hawataki asimamie uchaguzi kwa madai ameshindwa kutekeleza majukumu yake ikiwamo kutoa uamuzi wa kuzuia kampeni za Chadema kinyume cha utaratibu.
Mwanasheria wa chama hicho, kanda ya Pwani, Gaston Garubi amesema Kayombo hafai kusimamia uchaguzi kwa sababu ameonyesha wazi kuipendelea CCM huku akijua yeye ni mtumishi wa umma.

No comments:

Post a Comment