Thursday, November 23

Canada yatoa Sh14 bilioni kwa mpango wa uzazi


Zaidi ya wanawake milioni moja wanatarajia kunufaika na mpango wa uzazi salama na afya ya mtoto, baada ya ubalozi wa Canada nchini kutoa Sh114.2 bilioni kwa ajili ya mpango huo.
Mpango huo utakaotekelezwa na mashirika matano ya Aga Khan Foundation Canada, Amref, Care Canada, World Vision na Plan Intenational, utawanufaisha wanawake katika mikoa ya Tabora, Mwanza, Simiyu, Rukwa na Kigoma.
Akizindua mpango huo juzi, balozi wa Canada nchini, Ian Myles akiwa ameambatana na waziri wa afya, Ummy Mwalimu alisema lengo la mpango huo ni kuboresha afya ya mama na mtoto katika mikoa hiyo yenye changamoto.
Balozi Myles alisema mchakato huo utakwenda sambamba na utoaji mafunzo kwa watumishi wa afya na kuongeza vifaatiba, ili kupata matokeo mazuri.
“Canada itaendelea kuwa mdau wa mpango wa uzazi salama na afya ya mtoto. Pia, tunasaidiana na Serikali katika jitihada za kupunguza kiwango cha vifo vinavyotokana na uzazi,” alisema Balozi Myles.
Naye Mwalimu aliushukuru Ubalozi wa Canada kwa kushiriki kikamilifu katika jitihada za kuhakikisha mpango wa uzazi salama na afya ya mtoto unazidi kuboreshwa.
Alitumia nafasi hiyo kuyaasa mashirika yanayotekeleza mpango huo kutumia fedha hizo kwa uangalifu, sanjari na kushirikiana na Serikali hasa katika ngazi ya mkoa na halmashauri.
Mkurugenzi wa miradi wa World Vision, Revocatus Kamala alisema katika fedha hizo shirika hilo limepata Sh20 bilioni kwa ajili ya kutekeleza mradi huo Kigoma.
“Tutajikita katika kuimarisha mfumo wa uzazi bora na afya ya mtoto katika wilaya zote za Kigoma kwa miaka minne. Pia, tutajenga wodi za akina mama na chumba cha upasuaji,” alisema Kamala.
Naye mkurugenzi mkazi wa Plan International Tanzania, Jorgen Haldorsen alisema shirika hilo linafurahishwa kufanya kazi na Serikali ya Canada katika kutekeleza mpango huo mkoa wa Rukwa.

No comments:

Post a Comment