Thursday, November 23

Uchumi wa viwanda uendane na ujenzi wa maabara za Sekondari

Joseph Alphonce  ni Mtakwimu na Ofisa Mipango.
Joseph Alphonce  ni Mtakwimu na Ofisa Mipango. Anapatikana kwa 0685214949/0744782880. 
Dhima kuu ya ujenzi wa maabara kwa kila shule ya sekondari ya Serikili ilikuwa kuhakikisha Tanzania inazalisha wanasayansi, pamoja na mambo mengine, watakaotumika kufundisha wengine, kusimamia na kuendesha viwanda na kubuni, kuimarisha teknolojia.
Maendeleo ya teknolojia na ukuaji wa uchumi ni mambo yanayotegemeana. Huwezi kukuza uchumi kwa kasi kama teknolojia inayotumika ni ya zamani. Na huwezi kumudu kununua teknolojia mpya kila inapotoka kama nguvu yako kiuchumi si nzuri.
Maendeleo endelevu ya uchumi ni mchakato, hayawezi yakatokea mara moja kwa wakati mmoja. Katika mchakato huo wanasayansi ni moja ya kundi ambalo haliwezi kuepukwa au kutopewa kipaumbele kutokana na mchango wao wa kutatua changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza kwenye uzalishji w amali na huduma.
Ni kundi ambalo lina mchango mkubwa wa kuisaidia na kuelekeza Serikali masuala yote yahusuyo sayansi na teknolojia. Kwa Tanzania kundi hili limekuwa likipewa kipaumbele kwenye elimu ya juu ambako wanafunzi wanaochagua kozi zake hupata mkopo kwa asilimia 100 na uhakika wa ajira pale wanapohitimu masomo au mafunzo yao.
Katika maeneo mengi, ujenzi wa maabara ulisitishwa tangu mwaka 2015 kabla ya uchaguzi mkuu. Baada ya uchaguzi huo wa Oktoba, 2015 baadhi ya maeneo ukamilishaji ulisimama na sehemu nyingine unaendekea kwa kusuasua. Pengine viongozi wa maeneo husika wanasubiri maelekezo ya Serikali.
Maabara hizi kwa zaidi ya asilimia 60 zilijengwa kwa nguvu za wananchi wanaoamini zitawasaidia watoto wao kujifunza masomo ya sayansi kwa vitendo. Pengine uwapo wa maabara hizo ingekuwa fursa kwa watoto wa masikini na wanyonge kupenda masomo ya sayansi hivyo kuja kuwa faida kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi katika familia zao na taifa kwa ujumla.
Ujenzi wa maabara upo katika hatua mbalimbali za ukamilishaji katika maeneo tofauti nchini. Ni kazi yetu tuliobahatika kupata elimu kuitumia kwa wanufaa ya nchi. Pamoja na mambo mengine, kuishauri Serikali namna nzuri ya kutumia rasilimali tulizonazo kufikia maendeleo ya uchumi wa viwanda na kuondoa umasikini miongoni mwa Watanzania.
Zipo faida nyingi zitokanazo na kukamilishwa maabara za sekondari nchini. Mosi, watoto wa masikini na wanyonge ambao wengi wapo katika shule za kata watapata nafasi ya kusoma masomo ya sayansi kwa vitendo hivyo kuwa chachu ya kuzalisha wanasayansi wengi kutoka katika kundi kubwa la Watanzania kuliko ilivyo sasa.
Vilevile, wananchi wenyewe watakuwa na uwezo wa kubuni, kutengeneza, kuendesha na kusimamia mifumo ya kisayansi na teknolojia katika maeneo mbalimbali ikiwamo kwenye viwanda na mengine ya uwekezaji wa kimakakti.
Tatu, endapo uratibu huo utafanikiwa katika kipindi kirefu kijacho, Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi zinazoingiza fedha nyingi za kigeni kwa kuuza teknolojia katika nchi nyingine zenye uihitaji.
Serikali imekiri mara kadhaa kuwa Tanzania ina walimu wengi wa masomo ya sanaa kiasi cha baadhi yao kukosa vipindi hivyo kujielekeza kufanya shughuli binafsi muda wa kazi ikiwemo kuendesha “bodaboda.”
Aidha, ajira kwa walimu wa masomo ya sanaa zimekuwa za kusuasua kwani kuhitajika kwao kumekuwa kukipungua siku hadi siku tofauti na ilivyo kwa walimu wa masomo ya sayansi.
Serikali inaweza kuweka mpango kabambe kuhakikisha ujenzi wa maabara ambao umetumia rasilimali za wananchi wanyonge ikiwamo nguvu na michango yao ya vifaa au fedha zinaendelezwa kwa kutimiza lengo lililokusudiwa.
Takwimu zinaonyesha zaidi ya asilimia 50 ya wanafunzi wanaosoma katika shule za Serikali walikuwa wanakaa chini, baada ya Serikali kuamua, imewezekana hivyo kutengeneza madawati yaliyokidhi mahitaji yaliyopo na suala hilo sasa ni historia.
Ukuaji wa uchumi ni dhana pana, inahitaji ufanisi na uwajibikaji wa maeneo mengi. Elimu, hasa ya sayansi na teknolojia ni eneo ambalo linahitaji uwekezaji mkubwa ili uchumi wa viwanda ujengwe na kusimamiwa na Watanzania walio wengi.
Hapa hakuna mbadala. Lazima tuwe na teknolojia yetu itakayoturuhusu kuboresha uzalishaji kila itakapohitajika na kuhsindana kimataifa. Kitu kimoja tunapaswa kufahamu, huwezi kushindana na aliyekuuzia teknolojia kwakuwa yeye anafahamu zaidi udhaifu uliopo kwenye mitambo au mashine unazozitumia.
Kushindana na mataifa mengine yenye uchumi imara na yaliyoendelea kwa viwanda, mapinduzi ya sayansi na teknolojia hayakwepeki jambo ambalo litafanikishwa na vijana.
Maabara ni miongoni mwa sehemu sahihi kufanikisha ubunifu wa kazi za teknolojia hivyo ni muhimu kila shule ikawa nazo kuwapa vijana wote wa Kitanzania fursa ya kujaribu kutafuta suluhu ya kero zilizopo kwenye jamii.
Shule ambazo hazijakamilisha ujenzi zifanye hivyo hima ili asiachwe yeyote kwenye mchakato huu.
Mwandishi ni Mtakwimu na Ofisa Mipango.

No comments:

Post a Comment