Fedha hizo zilikabidhiwa kwa walimu hao kwa kipindi cha kati ya miaka miwili.
Inadaiwa kuwa walimu hao walikuwa wakipokea fedha kutoka kwa wazazi kati ya Sh2.4 milioni kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne na Sh3.5 milioni kwa wale wa kidato cha tano na sita.
Hata hivyo fedha hizo walikuwa wakizipokea bila kuziingiza kwenye akaunti ya shule iliyopo Benki ya NBC, tawi la Mwanza.
Badala yake, mwalimu Yusuph Sabato (46) na mwenzake Kenendy Odera (39) walighushi hati za malipo ya benki (pay-in-slips) na kuzikabidhi kwa wazazi ambao nao bila kujua, huziwasilisha idara ya uhasibu ya shule na kupewa stakabadhi za malipo ya ada na gharama zingine za masomo ya watoto wao. “Tayari tumelifikisha suala hilo polisi kwa sababu linahusiana na kosa la jinai la kughushi pay-in-slips na mihuri ya benki,” alisema James Bwire, mkurugenzi wa mtandao wa Taasisi ya Alliance inayomiliki shule hiyo.
Akizungumza na Mwananchi ofisini kwake juzi, Bwire ambaye pia ni meya wa Jiji la Mwanza alisema kwa sasa uongozi wa shule unajiepusha kuzungumzia suala hilo kwa undani ili kutoingilia upelelezi. “Kwa kifupi suala hilo lipo na linachunguzwa na vyombo vya dola kubaini wahusika, siwezi kulizungumzia kwa undani,” alisisitiza. Wanafunzi waliokumbwa na kadhia hiyo wanasoma kidato cha pili, tatu, nne, tano na sita na baadhi walijikuta wakisimamishwa masomo tangu Oktoba 14, kwa kosa la kutolipa ada, licha ya wazazi wao kulipa na kuwasilisha hati za malipo (zilizobainika ni za kughushi) na kupewa stakabadhi za shule.
Kauli ya polisi
Akizungumzia sakata hilo, kaimu kamada wa polisi mkoa wa Mwanza, Faustine Shilogile alisema uchunguzi wa kina unaendelea kubaini mtandao uliohusika kughushi nyaraka na mihuri ya benki baada ya uongozi wa taasisi hiyo ya fedha kuzikana.
Huku akiwasiliana kwa njia ya simu na mtu aliyemtaja kwa jina la Masaga aliyesema ndiye mpelelezi wa kesi hiyo, Shilogile aliahidi kuwa polisi itatoa taarifa zaidi kuhusu suala hilo baada ya upelelezi kukamilika.
Wazazi ‘walivyopigwa’
Baadhi wazazi waliozungumza na gazeti hili walisema kwa kipindi chote wamekuwa wakilipia gharama zote za elimu kuanzia ada na masomo ya ziada kupitia kwa walimu hao.
“Taarifa za mwanangu kudaiwa karo ya miaka miwili ni za kushtua kwa sababu nimelipa na kuwasilisha stakabadhi ya malipo ya benki shuleni na kupewa stakabadhi ya shule,” alisema Hawa Salum, mkazi wa Katoro wilayani Geita.
Akizungumza katika ofisi za gazeti hili jijini Mwanza mwishoni mwa wiki, Hawa alimtaja mwalimu Sabato wanayetoka wote wilayani Kasulu mkoani Kigoma kuwa ndiye aliyekuwa akipokea fedha kwa lengo la kumsadia kuzipeleka Benki ya NBC kutokana na benki hiyo kutokuwa na tawi Katoro.
“Nilifahamiana naye (mwalimu Sabato) nilipofika shuleni kumpeleka mwanangu Twalha Tawasul anayesoma kidato cha tatu, kwa miaka miwili nimtumia fedha anisaidie kulipa kutokana benki kuwa mbali nami. Inaniuma mimi na mwanangu kuwekwa mahabusu kwa tuhuma za kughushi hati za malipo ya benki,” alisema. “Wazazi tumejinyima kulipia ada na gharama zingine ili mtoto wetu apate elimu bora. Mungu atatulipia kisasi.”
Huku akibubujikwa na machozi wakati wa mahojiano hayo, mzazi huyo alisema hadi suala hilo linagundulika tayari mwalimu Sabato alishatia kibindoni zaidi ya Sh4.5 milioni ikiwa ni malipo ya ada na gharama za masomo ya ziada kwa kipindi cha miaka miwili.
Naye Athanas Awabu ambaye ni mzazi wa Salome Awabu, anayesoma kidato cha nne alikuwa akimkabidhi fedha Sabato ili azipeleke benki na kumpatia hati ya malipo alizokuwa akiziwasilisha shuleni ambazo sasa zimebainika zilighushiwa. Mzazi mwingine, mtumishi wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa gazetini alisema kwa miaka miwili, mwalimu Odera amekuwa akipokea fedha za malipo ya ada na gharama zingine za masomo ya mwanaye, Jenipher Masamba anayesoma kidato cha sita shuleni hapo. “Kwa kipindi chote hicho, amepokea zaidi ya Sh7.9 milioni. Amekiri na kukubali kuzirejesha. Nashukuru mwanangu ameruhusiwa kuendelea na masomo,” alisema mzazi huyo.
Walimu hao wanasemaje?
Akizungumza katika ofisi za gazeti hili jijini Mwanza juzi, mwalimu Sabato alikiri kupokea fedha kutoka kwa baadhi ya wazazi, naye akazikabidhi kwa mwenzake Odera ili azipeleke benki. “Naye (Odera) alikuwa akileta slips za benki. Nilizikabidhi kwa wahusika ambao nao waliziwasilisha idara ya uhasibu na kupewa stakabadhi za malipo za shule,” alisema Sabato.
Mwalimu Odera aliyekuwepo wakati mwenzake akieleza hayo alikiri kupokea fedha hizo na kuzitumia kufidia madai yake ya zaidi ya Sh30 milioni alizodai kuwa anaudai uongozi wa shule. “Kweli nilipokea fedha hizo na kuzitumia kujilipa kama njia ya kuushinikiza uongozi (wa shule) kunilipa madai yangu. Nipo tayari kuzilipa kwa sharti la uongozi wa shule kunilipa madai yangu yote,” alisema Odero.
Hata hivyo, mwalimu huyo alikataa kujibu swali la wapi alipata hati za malipo na mihuri ya benki.
“Hilo la pay-in-slips na mhuri tuliache. Muhimu nitarejesha fedha zote kwa sharti la mimi pia kulipwa madai yangu,” alisema Odera.
Alipoulizwa iwapo kweli walimu hao wana madai dhidi ya uongozi wa shule hiyo, Bwire alisisitiza msimamo wake wa kutozungumzia suala hilo akisubiri uchunguzi wa polisi.
No comments:
Post a Comment